Breaking News

FERNANDO WOLLE ATANGAZA NIA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA KIKABWE KWA TIKETI YA CCM

Mtia nia wa Ubunge Jimbo la Kibakwe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fernando Wolle, ametangaza rasmi azma yake ya kulitumikia jimbo hilo kwa moyo, maarifa na uadilifu, akiahidi kuleta taswira mpya ya maendeleo na uwakilishi jumuishi.

Fernando Wolle, mzaliwa wa kata ya Ipera, Jimbo la Kibakwe, ni kijana mwenye historia ya ukakamavu, elimu na uaminifu kwa itikadi ya CCM. Ni mhitimu wa Shahada ya Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (2015), na aliwahi kuhudumu kama Mwandishi wa Habari katika magazeti ya The African na Mtanzania kati ya mwaka 2014 na 2015.

Katika taaluma yake, Wolle amejijengea uzoefu mkubwa katika mawasiliano na uongozi, akihudumu kama Meneja wa Masoko na Mawasiliano katika kampuni ya kimataifa ya Transsion Holdings (itel na TECNO) kuanzia mwaka 2016 hadi 2024. Hivi karibuni, alihudumu kama Afisa Masoko ya Kimtandao katika kampuni ya Hisense.
Safari yake ya kiutendaji ilianza mapema mwaka 2010/2011 akiwa Mwalimu wa kujitolea katika shule ya sekondari ya Itiso wilayani Chamwino, akifundisha masomo ya Lugha na Historia hatua inayodhihirisha dhamira yake ya utumishi kwa jamii.

Kwa kuzingatia uzoefu wake katika mawasiliano, Wolle anaamini kuwa msingi wa maendeleo ni mawasiliano bora kati ya wananchi na viongozi. “Mawasiliano yanayojenga mshikamano, uwajibikaji na maendeleo ni nguzo ya mafanikio ya kweli ya wananchi wa Kibakwe,” amesisitiza.

Katika kampeni yake, Fernando Wolle amejipambanua kwa sera zinazolenga maendeleo jumuishi, ushirikishwaji wa vijana na wanawake, uwazi na uwajibikaji, pamoja na kulinda rasilimali za jimbo hilo kwa manufaa ya wazawa. Aidha, amedhamiria kuimarisha huduma za jamii kama afya, maji na elimu ili Kibakwe iwe mfano wa kitaifa.

Anasisitiza pia umuhimu wa kubuni fursa za kiuchumi kupitia miundombinu ya kudumu itakayokiunganisha Kibakwe na maeneo yenye uchumi unaokua kama mikoa jirani na miji mikuu.

Kwa kaulimbiu yake isemayo: “Kibakwe... Akili Mpya, Taswira Mpya na Mwelekeo Mpya,” Wolle anaamini kuwa wakati wa mabadiliko yenye maono umefika na yeye ndiye sauti ya waliopuuzwa kwa muda mrefu.