MEYA SONGOLO AISHUKURU SERIKALI KWA MAFANIKIO YA MIRADI YA MAENDELEO
Dar es Salaam - Meya wa Wilaya ya Kinondoni, Songolo Mnyonge, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendeleza miradi ya maendeleo katika kata zote 20 za wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kuvunja Baraza la Madiwani la wilaya hiyo, Mnyonge amesema wanaondoka wakiwa wameridhika na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo imeiwezesha Manispaa ya Kinondoni kuwa imara katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Katika kipindi cha miaka mitano, tumeshuhudia mafanikio mengi. Mafanikio haya hayakuja kwa bahati mbaya, bali yametokana na ushirikiano madhubuti kati ya baraza la madiwani na serikali,” alisema Songolo.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na usimamizi mzuri, ushirikiano na uaminifu miongoni mwa viongozi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Katika hatua nyingine, Songolo amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ya kulinda amani na umoja katika wilaya hiyo. “Tunajivunia umoja, amani na usalama katika wilaya yetu, na haya ni matokeo ya uimara wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama,” aliongeza.
Aidha, amepongeza hatua ya kuimarisha miundombinu ikiwemo uwepo wa magreda matatu yanayofanya kazi kwa sasa, na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuendelea kuyasimamia pamoja na kushughulikia miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua zilizonyesha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni, Bi Hanifa Hamza, amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 yametokana na ushirikiano mzuri kutoka kwa Baraza la Madiwani.
“Baraza hili limekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya halmashauri yetu. Miradi mbalimbali imetekelezwa ikiwemo ujenzi wa jengo la halmashauri. Ni matumaini yangu kuwa baraza lijalo nitaendelea kuwaona madiwani hawa ili tuendelee kuleta maendeleo kwa wananchi wetu,” alisema Hanifa.
Amesisitiza kuwa ofisi yake itaendelea kusimamia ipasavyo miradi yote ya maendeleo inayoendelea, na kutoa mrejesho kwenye baraza lijalo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni amewapongeza madiwani hao kwa kutekeleza kikamilifu Ilani ya chama hicho, akisema kazi yao imekifanya chama kiheshimike.
“Chama kimeridhishwa na utendaji wa madiwani hawa. Miradi yote imepitia katika vikao vya chama na tumeridhika na utekelezaji wa Ilani yetu,” alisema mwenyekiti huyo.






