Breaking News

JMAT KUFANYA MATEMBEZI YA AMANI DAR – DODOMA NA KUZINDUA KITABU CHA 4R ZA MAMA

Dar es salaam - Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imetangaza kufanya matembezi ya kihistoria ya hiari, yajulikanayo kama Matembezi ya Hiari ya Amani (MHA), yatakayoanzia jijini Dar es Salaam hadi makao makuu ya serikali jijini Dodoma. Matembezi hayo yatafanyika kwa siku 20 kuanzia Juni 19 hadi Julai 9, 2025, yakihusisha umbali wa takriban kilomita 452.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 10, 2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa JMAT Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum alisema matembezi hayo yatahusisha washiriki zaidi ya 300 watakaotembea kwa miguu kwa lengo la kuhamasisha amani kuelekea uchaguzi mkuu, kuwaelimisha wananchi kuhusu mbinu za kulinda amani, pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta za kilimo, viwanda, na madini.

Uzinduzi rasmi wa matembezi hayo utafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na unatarajiwa kufanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Washiriki wa matembezi watapita katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kiluvya, Misugusugu, Vigwaza, Chalinze, Ubena Zomozi, Mikese, Morogoro Mjini, Mvomero, Wami Dakawa, Dumila, Maguha, Kiyegeya, Gairo, Kibaigwa, Chamwino Ikulu hadi kufikia Dodoma Mjini.

Matembezi hayo yatahitimishwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika maeneo mbalimbali watakapopitia, kutafanyika mikutano ya hadhara minne kwa ajili ya kuelimisha wananchi juu ya amani na ushiriki wa uchaguzi. Vilevile, kutakuwa na makongamano ya ndani katika vituo vinane kwa lengo la kutoa elimu ya kina kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini.

Aidha, JMAT pia inatarajia kuzindua kitabu kipya kiitwacho “4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan” kinachochambua mchango wa Rais Samia katika kuimarisha utulivu, amani na mahusiano ya kitaifa na kimataifa. Uzinduzi wa kitabu hicho utafanyika Juni 22, 2025 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 hadi saa 4:00 usiku. Kitabu hicho kimeandikwa na wanazuoni wa dini zote mbili pamoja na maprofesa kutoka sekta mbalimbali.

Katika hatua nyingine, JMAT imethibitisha kuwa itashiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba mwaka huu, ambapo watakuwa na banda lao maalum litakalotumika kuonesha mchango wa viongozi mbalimbali katika kuimarisha amani ya Taifa.