WAZIRI MKUU MGENI RASMI UZINDUZI WA SAMIA LEGAL AID DSM
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid) itakayofanyika katika viwanja vya Maturubai, Mbagala, Wilaya ya Temeke kuanzia Juni 16 hadi Juni 25, 2025.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Ester Msambazi, akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid) itakayofanyika katika viwanja vya Maturubai, Mbagala, Wilaya ya Temeke kuanzia Juni 16 hadi Juni 25, 2025.
Dar es Salaam – Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid) itakayofanyika katika viwanja vya Maturubai, Mbagala, Wilaya ya Temeke kuanzia Juni 16 hadi Juni 25, 2025.
Akizungumza leo, Juni 13, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kampeni hiyo yenye lengo la kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria, ikiwemo migogoro ya ardhi na masuala ya ukatili wa kijinsia.
“Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Wizara ya Katiba na Sheria, chini ya udhamini wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Natoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kupata msaada wa kisheria,” alisema Mhe. Chalamila.
Ameeleza kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuwasaidia wananchi kushughulikia kero na changamoto za kisheria ili kuimarisha haki, usawa, amani na maendeleo ya jamii. Amewahimiza wananchi wenye matatizo ya kisheria kutumia fursa hiyo.
Aidha, Mhe. Chalamila ameongeza kuwa Jiji la Dar es Salaam limekuwa moja ya maeneo yenye migogoro mingi, hasa ya ardhi na ukatili wa kijinsia, hivyo kutakuwepo na wataalamu wa sheria pamoja na madawati ya kijinsia kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Ester Msambazi, amesema kuwa kampeni hiyo ilianza kutekelezwa mwaka 2023 na tayari imefika katika mikoa yote mitano ya Zanzibar na mikoa 25 ya Tanzania Bara, ikiwa imeshawahudumia na kuwasaidia zaidi ya wananchi milioni 2.





