MWENYEKITI WA INEC ATEMBELEA MAGEREZA KUKAGUA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mheshimiwa Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, leo Juni 28, 2025, ametembelea na kukagua mwenendo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Magereza ya Bukoba, Muleba, Biharamulo mkoani Kagera, pamoja na Gereza la Chato lililopo mkoani Geita.
Ziara hiyo imefanyika sambamba na uzinduzi wa mzunguko wa tatu wa awamu ya pili ya zoezi la uboreshaji wa Daftari hilo kwa wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya miezi sita pamoja na mahabusu walioko katika Magereza ya Tanzania Bara na katika Vyuo vya Mafunzo Zanzibar
Zoezi hilo limeanza rasmi leo Juni 28, 2025, na linatarajiwa kuendelea kwa muda wa siku saba hadi Julai 04, 2025.
Katika ukaguzi wake, Mhe. Jaji Mwambegele amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa ya kujiandikisha anapata haki yake ya msingi ya kushiriki kwenye chaguzi mbalimbali za kidemokrasia nchini. Pia amezitaka mamlaka husika kushirikiana kwa karibu na Tume ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Zoezi hili ni sehemu ya juhudi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha ushiriki jumuishi katika mchakato wa kidemokrasia kwa makundi yote ya jamii, ikiwemo wafungwa na mahabusu wanaostahili kwa mujibu wa sheria.








