Breaking News

RC CHALAMILA AKAGUA UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI, KIGOGO NA MKWAJUNI

Dar es Salaam – Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amefanya ukaguzi wa ujenzi wa daraja la kudumu la Jangwani pamoja na madaraja ya muda yanayojengwa katika maeneo ya Kigogo na Mkwajuni. Madaraja haya ya muda yanatarajiwa kusaidia wananchi wakati wa ujenzi wa daraja kuu la Jangwani.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Chalamila amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), na amemtaka mkandarasi kuhakikisha kazi inafanyika kwa ubora wa hali ya juu na kwa saa 24 ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Amesema kuwa eneo la Jangwani limekuwa likikumbwa na mafuriko kila msimu wa mvua, hivyo ujenzi wa daraja hilo ni suluhisho la kudumu kwa wananchi. Aidha, amefafanua kuwa serikali tayari imeshatoa shilingi bilioni 14 kati ya bilioni 97 zinazohitajika kukamilisha mradi huo.

Katika ziara hiyo, RC Chalamila pia aliagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha uwanja wa mikutano wa Jangwani unarejeshwa ili uendelee kutumika kwa shughuli za kijamii kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kwa upande wao, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, walimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kugharamia mradi huo. Walisema ujenzi wa daraja hilo na madaraja ya muda utasaidia kuondoa kero ya mafuriko na kurahisisha usafiri kwa wananchi.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Eng. Lazerk Kyamba, alieleza kuwa ujenzi wa daraja la Jangwani utachukua miezi 24 na kugharimu shilingi bilioni 97. Kwa sasa maandalizi ya mradi huo yamefikia asilimia 7. Aidha, ujenzi wa madaraja ya muda katika maeneo ya Kigogo na Mkwajuni unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 10, na barabara maalum ya dharura pia itajengwa kupitisha magari wakati wa ujenzi wa daraja kuu.

Ujenzi wa daraja la Jangwani unalenga kutatua changamoto za muda mrefu za mafuriko na kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao bila usumbufu wakati wa mvua.