Breaking News

RC CHALAMILA: WAKAZI WA DAR ES SALAAM JITOKEZENI KWA WINGI KUNUFAIKA NA MSAADA WA KISHERIA BILA MALIPO

Dar es Salaam — Wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanatarajiwa kunufaika na msaada wa kisheria bure kupitia kampeni ya “Mama Samia Legal Aid” itakayoendeshwa kwa siku 10 mfululizo kuanzia Jumatatu, Juni 16, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema shughuli hiyo ya utoaji wa msaada wa kisheria itazinduliwa rasmi katika viwanja vya Maturubai, Mbagala, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (MB).

“Napenda niwafahamishe wakazi wa Dar es Salaam kuwa kampeni hii itazinduliwa siku hiyo na baadaye kuendelea katika Halmashauri zote za Mkoa huu,” alisema Mhe. Chalamila.

Kwa mujibu wa Mhe. Chalamila, huduma zitakazotolewa katika kampeni hiyo ni pamoja na usaidizi wa kisheria kuhusu mirathi, migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa, uandishi wa wosia, na huduma nyingine za kisheria zitakazotolewa na wataalamu wa sheria waliobobea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Ester Msambazi, amesema kuwa kampeni hii inalenga kusaidia wananchi wenye kipato cha chini ambao wamekuwa wakikosa huduma za kisheria kutokana na changamoto za kiuchumi na uelewa mdogo kuhusu haki zao.

“Kampeni hii ya Mama Samia Legal Aid ni mkakati mahsusi wa Serikali wa kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata haki kupitia huduma ya msaada wa kisheria bila vikwazo vya kiuchumi,” alisema Bi. Msambazi.

Wananchi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma hizo zitakazokuwa zikitolewa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi chote cha kampeni.