Breaking News

SERIKALI YAZINDUA RIPOTI YA MAHITAJI YA TEKNOLOJIA (TNA) KWA MAENDELEO YA UCHUMI WA KISASA

Dar es Salaam – Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa kwa Nchi Zinazoendelea (LDCs), imezindua rasmi Ripoti ya Tathmini ya Mahitaji ya Teknolojia (TNA), ikiwa ni hatua muhimu katika safari ya kuelekea uchumi wa kisasa unaotegemea ubunifu, sayansi na teknolojia.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau kutoka sekta ya umma, binafsi na taasisi za kimataifa. Ripoti hiyo inalenga kubaini teknolojia muhimu zitakazochochea maendeleo katika sekta za kilimo na uchumi wa buluu—ambazo ni nguzo kuu za maisha ya Watanzania walio wengi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Shaban Ali Othman, alisema ripoti ya TNA ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya wakulima wa mwani na wafugaji wa samaki.

“TNA imeweka wazi ni teknolojia gani tunahitaji, lini na kwa namna gani zitasaidia kuongeza tija kwa wananchi wetu. Teknolojia kama mifumo ya dijitali ya usimamizi wa kilimo na uvuvi zitaboresha maisha ya wengi,” alisema Waziri Othman.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, alieleza kuwa TNA si tu nyaraka bali ni dira ya maendeleo ya kiteknolojia kwa nchi zinazoendelea.

“Teknolojia zikiwekwa kipaumbele, zinaweza kubadili maisha kwa kuongeza usalama wa chakula, kukuza ajira kwa vijana na wanawake, na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Komatsubara.

Alihimiza mashirika ya maendeleo, sekta binafsi na serikali kutafsiri mapendekezo ya ripoti hiyo kuwa miradi ya vitendo kwa manufaa ya taifa.
Naye Mwakilishi wa Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa, Bw. Deodat Maharaj, alibainisha kuwa ripoti hiyo imeainisha maeneo yenye fursa kubwa za ukuaji kama vile nishati mbadala, majukwaa ya kidijitali kwa kilimo na teknolojia za kisasa za uvuvi.

“Tanzania ina zaidi ya kilomita 1,400 za fukwe—hii ni hazina. TNA imeonesha njia sahihi ya kuwekeza na kutumia teknolojia kama injini ya maendeleo,” alisema Maharaj.

Ripoti ya TNA imepokelewa kwa mikono miwili kama chachu ya mageuzi ya kiuchumi. Serikali na Umoja wa Mataifa wameahidi kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa mapendekezo hayo kupitia miradi ya pamoja, usaidizi wa kiufundi na uwezeshaji wa jamii.