SADC YADHAMILRIA KUKOMESHA UJANGILI NA KUBORESHA HUDUMA KWA WAKIMBIZI
Na Neeema Mpaka, Dar es Salaam – Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Maduhu Isaac Kazi, amesema nchi wanachama wa SADC wamekubaliana kushirikiana kwa karibu ili kukabiliana na vitendo vya ujangili wa wanyamapori na kuhakikisha ulinzi madhubuti wa rasilimali hizo muhimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo baada ya kikao cha viongozi wa SADC, Dkt. Maduhu amesema mkutano huo umeweka mkazo katika utunzaji wa wanyamapori kwenye maeneo yote ya hifadhi, huku akibainisha kuwa hatua za pamoja zimewekwa kuhakikisha usalama wa wanyamapori dhidi ya majangili.
“Kuna makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kuhusu namna ya kukabiliana na majangili wanaoingia kwenye maeneo ya wanyamapori wetu. Tumeamua kushirikiana kwa karibu kama nchi wanachama ili kuhakikisha wanyamapori wetu wanakuwa salama,” alisema Dkt. Maduhu.
Aidha, mkutano huo umejadili masuala mengine muhimu yakiwemo uhamiaji na huduma kwa wakimbizi, kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika ukanda wa SADC.
Akizungumzia suala la uhamiaji, Dkt. Maduhu amesema nchi wanachama zimeweka taratibu bora kwa watu wanaohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kuhakikisha wanapata huduma bila vikwazo.
“Kuhusu wakimbizi, tunawasaidia kwa ukaribu ili waweze kufika salama katika maeneo wanayoelekea na pia kuhakikisha wanarudi katika nchi zao wakiwa salama na kuendelea na shughuli zao,” aliongeza Dkt. Maduhu.
Mkutano huo umehudhuriwa na wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 10 wanachama wa SADC, zikiwemo Tanzania, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Namibia, Angola, Afrika Kusini na nyinginezo.




