Breaking News

SHEIKH MKUU WA SHIA ITHNAASHARIYYAH ASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 20 YA CHUO KIKUU CHA KIISLAM MOROGORO

Morogoro - Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithnaashariyyah Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, ameshiriki katika maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (Muslim University of Morogoro – MUM).

Maadhimisho hayo yamefanyika kwa mafanikio makubwa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Kassim, ambaye aliwaongoza wageni waalikwa katika kusherehekea mafanikio ya chuo hicho kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.
Katika hafla hiyo, Maulana Sheikh Hemedi Jalala alitumia fursa hiyo kupongeza chuo kwa mchango wake mkubwa katika kuelimisha jamii na kuendeleza maadili mema ya Kiislamu. Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi za dini katika kuimarisha elimu, amani, na mshikamano wa kitaifa.

Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro kimekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya elimu nchini, kikiwapatia vijana elimu bora inayochanganya maarifa ya kidunia na misingi ya kiroho, hivyo kuwaandaa kuwa raia wema na wachangiaji wakuu katika maendeleo ya taifa.