Breaking News

TANZANIA KUWA WENYEJI WA JUKWAA KUBWA LA AKILI BANDIA (AI) 2025

Dar es Salaam, Tanzania – Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Tume ya TEHAMA (ICT Commission – ICTC) inaleta Jukwaa kubwa la Akili Bandia (AI), linalotarajiwa kufanyika tarehe 28-29 Julai 2025 jijini Dar es Salaam.

Tukio hili la kihistoria linalenga kukutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali zikiwemo serikali, sekta binafsi, vyuo vikuu, wajasiriamali, wanafunzi, wakulima na makundi mengine ya kijamii yanayonufaika na teknolojia ya AI. Jukwaa hili linatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya majadiliano ya kitaifa kuhusu matumizi ya AI kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa ICTC, Dkt. Nkundwe Mwasaga, ameeleza kuwa Akili Bandia tayari ina mchango mkubwa nchini, ikitumiwa katika Mahakama ya Tanzania, taasisi za elimu, sekta ya afya na maeneo mengine muhimu. “Hiki ni kipindi muhimu cha mabadiliko ya kiteknolojia. AI ni chachu ya maendeleo jumuishi, lakini ni lazima itumike kwa kuzingatia maadili yetu ya Kitanzania na misingi ya utawala wa taarifa,” alisema Dkt. Mwasaga.

Kauli mbiu ya jukwaa hili ni: “Tunatengeneza Kesho ya Tanzania inayotumia Akili Bandia inayofuata Maadili yetu na Utawala wa Taarifa kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii.”

Katika jukwaa hilo, washiriki watajadili masuala ya msingi yanayohusu AI, ikiwa ni pamoja na:

Maadili katika matumizi ya AI kwa mujibu wa utamaduni wa Kitanzania, Usalama na ulinzi wa taarifa binafsi, Fursa za kiuchumi zinazotokana na AI, Ubunifu wa ndani unaotumia teknolojia hii.

Serikali kupitia ICTC imeanza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kuanzisha vituo vya taarifa pamoja na kuandaa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ili kuhakikisha matumizi ya AI yanakuwa salama na jumuishi.

Jukwaa hili pia litatoa jukwaa la kuonesha bunifu za Watanzania katika AI, likiwa ni nafasi ya kipekee kwa vijana na wabunifu kuonesha kazi zao na kuunganishwa na fursa mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Wananchi wote wanakaribishwa kushiriki tukio hili la kihistoria litakaloweka msingi wa kesho ya kidijitali ya Tanzania.