Breaking News

WAANDISHI 400 WAJISAJILI BODI YA ITHIBATI

Dar Es salaam - Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amesema kuwa mwitikio wa waandishi wa habari kujisajili kwa njia ya kidijitali umeongezeka maradufu, ambapo hadi kufikia Juni 11, 2025, waandishi 400 walikuwa wamejisajili tangu mfumo huo kufunguliwa Mei 19, 2025.

Wakili Kipangula ametoa taarifa hiyo alipokuwa akizungumza na TBC katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri, jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa waandishi wanaojisajili kupitia Bodi hiyo hupata fursa ya mafunzo, kutambulika rasmi, na kufanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, maadili, na weledi ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amebainisha kuwa ifikapo Juni 21, 2025, waandishi wa habari ambao hawatakuwa wamejisajili hawataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi bila kuwa kwenye mfumo wa TAI-Habari.