CHACHA WAMBURA NCHAMA ACHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KIVULE KUPITIA CCM
Dar es Salaam, Julai 1, 2025 – Mwanasiasa Chacha Wambura Nchama amejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Jimbo la Kivule baada ya kuchukua fomu ya kugombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Nchama amechukua fomu hiyo leo mbele ya Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Chief Sylvester Yaredi, katika ofisi za chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Nchama amesema kuwa uamuzi wake wa kugombea nafasi hiyo umetokana na dhamira ya dhati ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika juhudi za kuondoa changamoto mbalimbali zinazolikabili Jimbo la Kivule.
"Nimetia nia kugombea ubunge si kwa ajili ya heshima binafsi, bali kwa ajili ya kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha changamoto za wananchi wa Kivule zinapatiwa suluhisho la kudumu," amesema Nchama.
Hatua hiyo inaashiria kuanza kwa harakati za ndani ya chama hicho kuelekea mchakato wa kura za maoni na hatimaye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.





