Breaking News

CHAUMMA: UTEUZI WA VIONGOZI WA VITI MAALUM KUZINGATIA MCHANGO HALISI WA WANAOGOMBEA

Dar es Salaam – Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salumu Mwalimu, amesema uteuzi wa wabunge na madiwani wa viti maalum ndani ya chama hicho utafanyika kwa kuzingatia mchango wa mgombea katika jimbo au kata husika, si kwa misingi ya urafiki, ukaribu au upendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam, Bw. Mwalimu alisisitiza kuwa nafasi hizo zitatolewa kwa wale waliothibitisha kujitoa kwa wananchi na kufanya kazi kwa bidii wakati wa uchaguzi.
“Mbunge au diwani wa viti maalum wa CHAUMMA atateuliwa kutokana na jasho alilolitoa katika jimbo au kata. Hatutatoa nafasi kwa watu waliokaa ofisini tu bila kujitoa kwa wananchi,” alisema.

Bw. Mwalimu aliongeza kuwa msimamo huo unalenga kuimarisha uwajibikaji, ushindani wa haki ndani ya chama, na kuhakikisha kuwa viongozi wa viti maalum wanawakilisha vyema maslahi ya wananchi waliowatuma.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo alipokea ripoti ya mapendekezo kuhusu sifa, vigezo na mchakato wa ndani ya chama wa upatikanaji wa wabunge, madiwani na wawakilishi wa viti maalum. Ripoti hiyo imeandaliwa na kamati ndogo iliyoundwa kwa ajili ya kukusanya maoni ya wanachama na viongozi wanawake kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao
Akizungumza wakati wa makikabidhi ya ripoti hiyo, Katibu wa Kamati hiyo, Bi. Moza Ally, alisema mapendekezo yaliyowasilishwa yatasaidia chama kuandaa vigezo bora zaidi vitakavyowezesha kupatikana kwa viongozi makini na wanaokubalika katika nafasi hizo.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa uteuzi wa viti maalum unazingatia uwezo, uadilifu na mapenzi ya kweli kwa wananchi,” alisema Bi. Moza.

Chama cha CHAUMMA kinatarajia kutumia mapendekezo hayo kama sehemu ya mikakati ya ndani kujiandaa kwa ushindani wa kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.