DCEA YAKAMATA ZAIDI YA KILO 37,000 ZA DAWA ZA KULEVYA NCHINI
Dar es Salaam — Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetangaza kukamata dawa za kulevya zenye uzito wa kilogramu 37,197.142 katika operesheni mbalimbali zilizofanyika nchini kati ya Mei hadi Julai mwaka huu.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri wa vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.
Katika ukamataji huo, kilo 11,031.42 za dawa mpya za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa (maarufu kama Kratom) zilikamatwa zikiwa zimeingizwa nchini kutoka Sri Lanka kupitia Bandari Kavu ya Temeke, zikifichwa kwenye vifungashio vilivyodaiwa kuwa vya mbolea. Dawa hiyo ina kemikali aina ya Mitragynine na 7-Hydroxy-mitragynine, ambazo huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu na hata vifo.
Aidha, dawa nyingine zilizokamatwa ni pamoja na bangi kilogramu 24,873.56, mirungi kilogramu 1,274.47, skanka kilogramu 13.42, heroin kilogramu 2.21, methamphetamine gramu 1.42, na dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya ketamine kilogramu 1.92 na vidonge 1,000 vya rohypnol (Flunitrazepam). Pia, lita sita za kemikali bashirifu aina ya hydrochloric acid zilinaswa.
Katika operesheni nyingine, kilo 26 za heroin zilikamatwa zikiwa katika harakati za kuingizwa nchini kutoka Msumbiji, huku jumla ya watuhumiwa 64 wakikamatwa kuhusiana na matukio haya.
Kamishna Lyimo alibainisha kuwa watuhumiwa sita, wakiwemo raia wawili wa China waliotajwa kwa majina ya Chein Bai na Qixian Xin, walikamatwa katika eneo la Posta jijini Dar es Salaam wakiwa na methamphetamine, ketamine, na vidonge vya rohypnol.
Katika mtaa wa Sinza jijini Dar es Salaam, watu wawili walikamatwa wakiwa wamiliki wa kiwanda bubu cha kutengeneza biskuti zenye bangi ambazo zilisambazwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara. Mfanyabiashara mmoja wa madini mkoani Lindi naye alikamatwa akisambaza biskuti zenye bangi.
Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora, Morogoro na Arusha ilishuhudia ukamataji wa kilo 26,191.45 za dawa za kulevya za mashambani na uteketezaji wa ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi.
Kamishna Lyimo alieleza pia kuhusu mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu, ikiwemo kutumia miili ya binadamu (maiti) kama njia ya kusafirisha dawa hizo. Aidha, raia wa kigeni wamekuwa wakiwatumia Watanzania kwa kuwahusisha kwenye usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya kwa kutumia vyombo kama bodaboda, bajaji, teksi, na hata kampuni zao za usafirishaji.
DCEA imewataka wananchi kuwa makini wanapotumwa au kupokea mizigo kutoka kwa watu wasiowafahamu vizuri ili kuepuka kujihusisha bila kujua na biashara ya dawa za kulevya.
"Ni muhimu kujiridhisha na mizigo inayosafirishwa ili kuepuka kuingia kwenye matatizo ya kisheria," alisema Lyimo na kusisitiza kuwa yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara hiyo, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
DCEA imewaomba Watanzania kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kutokomeza kabisa biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.




