KIJANA ALIYEDAIWA KUCHOMWA KISU MBAGALA: POLISI WATOA UFAFANUZI WA TUKIO
Dar es Salaam – Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa ufafanuzi kuhusu tukio la kijana kudaiwa kuchomwa visu na vijana wa mtaa mmoja katika eneo la Jeshini, Mbagala, lililosambaa kwenye mitandao ya kijamii kupitia video ya baba wa kijana huyo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Polisi, tukio hilo lilitokea tarehe 22 Juni 2025 majira ya saa 2 usiku ambapo Osama Khamis Mohamed (18), mkazi wa Mwembemtongo, Tuangoma, Temeke alijeruhiwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kisu baada ya kutokea ugomvi kati yake na vijana wenzake wanne kutoka mtaa mmoja. Chanzo cha ugomvi huo kilitajwa kuwa ni deni la shilingi 2,000/= ambapo majeruhi alidaiwa kiasi hicho, na aliposhindwa kulipa, simu yake ya mkononi ilinyang’anywa kwa nguvu.
Jeshi la Polisi limesema watuhumiwa wa tukio hilo ni Muhidini Yahaya, Musa Bakari, Adam Athuman na kijana mwingine. Wote walikamatwa baada ya tukio na kuhojiwa, tofauti na madai yaliyotolewa na baba wa majeruhi kuwa waliondolewa kituoni siku iliyofuata licha ya mtoto wake kuwa katika hali mbaya.
Majeruhi alipelekwa Zahanati ya Mala na baadaye Hospitali ya Temeke ambako alitibiwa na kuruhusiwa tarehe 23 Juni 2025 baada ya kuthibitika hali yake si mbaya kama ilivyodaiwa mitandaoni.
Tarehe 27 Juni 2025, watuhumiwa walipewa dhamana kwa mujibu wa sheria baada ya jalada kufikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Mmoja wa watuhumiwa, Muhidini Yahaya, alifikishwa mahakamani kwa kosa la kujeruhi (CC no. 16613/2025) mbele ya Hakimu Lukosi, akiwakilishwa na mwendesha mashtaka Jackline Werema. Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena tarehe 22 Julai 2025.
Polisi wameeleza kuwa uamuzi wa kutoa dhamana ulifikiwa kwa kuzingatia hali ya majeruhi ambaye tayari alikuwa ameruhusiwa hospitalini, pamoja na malalamiko kutoka kwa wazazi wa watuhumiwa kuwa mlalamikaji (baba wa kijana) aliwatisha na kudai kiasi cha shilingi milioni nne ili asiendelee kufuatilia kesi hiyo, jambo lililozua taharuki.
Aidha, Jeshi la Polisi limeanzisha uchunguzi dhidi ya askari mpelelezi Cpl. Monika kufuatia tuhuma za kutowajibika ipasavyo kama ilivyolalamikiwa.
Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuacha kutumia kesi kama chanzo cha mapato kwa kuwatisha au kuwadai fedha ndugu wa watuhumiwa. Limeahidi kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuepusha taharuki na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.




