Breaking News

DIWANI GODFREY MITI AJITOSA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO JIPYA LA CHATO KUSINI

Mwanasiasa machachari, Godfrey Miti, ambaye amehudumu kama diwani wa Kata ya Buseresere, Wilaya ya Chato tangu mwaka 2015 hadi 2025 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amechukua fomu ya kugombea ubunge katika Jimbo jipya la Chato Kusini.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Miti amesema uamuzi wake umetokana na nia ya kutumia uzoefu alioupata katika nafasi ya udiwani ili kulitumikia vyema jimbo hilo jipya, ambalo lilitangazwa mapema mwaka huu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Amesisitiza kuwa uongozi bora hupimwa kwa uwajibikaji na utekelezaji wa ilani ya chama kwa maslahi ya wananchi waliomchagua. Miti ameahidi kuendelea kuwa mtumishi mwaminifu wa wananchi na kusimamia maendeleo ya Chato Kusini endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge.

Jimbo la Chato Kusini ni miongoni mwa majimbo mapya yaliyoanzishwa kufuatia mabadiliko ya mipaka ya kiutawala yaliyofanywa na NEC ili kuongeza uwakilishi wa wananchi.