Breaking News

SHABAN MATWEBE ACHUKUA NA KUREJESHA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE RUFIJI KUPITIA CCM

Rufiji, Pwani – Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rufiji, Shaban Matwebe, hatimaye amekabidhiwa rasmi fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Rufiji katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025. Tukio hilo limehitimisha sintofahamu ya awali iliyozua gumzo katika eneo hilo.

Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Matwebe alieleza furaha yake kwa hatua hiyo muhimu, akisema: “Hatimaye nimepewa fomu, nimechukua, nimejaza. Na hapa sasa hivi ndo nimetoka kukabidhi fomu. Chama changu kimenipa nafasi ya kuingia kwenye mchakato. Na Mungu akipenda, Inshallah, jina likirudi, tuingie kwenye kivumbi na jasho.”
Hapo awali, Matwebe alikumbwa na hali ya sintofahamu baada ya kutajwa kuwa alinyimwa fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Rufiji, Prudence Sempa, bila kutolewa maelezo rasmi. Hali hiyo ilizua maswali miongoni mwa wafuasi wake na wanachama wa CCM katika jimbo hilo.

Matwebe ni miongoni mwa wagombea wanaotajwa kuwa na mvuto mkubwa kwa wapiga kura wa CCM katika Jimbo la Rufiji. Anatarajiwa kukabiliana na Mbunge anayemaliza muda wake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, ambaye naye tayari amechukua fomu ya kutetea nafasi hiyo.

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za maombi ya uteuzi ndani ya CCM linaendelea kote nchini kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.