Breaking News

DKT. MWASAGA AFUNGUA RASMI TANZANIA AI FORUM 2025, ASISITIZA MAADILI NA USHIRIKISHWAJI KATIKA MAPINDUZI YA KIDIJITALI

Dar es Salaam, Julai 28, 2025 — Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga, leo amefungua rasmi Mkutano wa kwanza wa kihistoria wa Tanzania Artificial Intelligence Forum 2025, akitoa dira ya maendeleo ya matumizi ya teknolojia ya Akili Bandia (AI) nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili, Dkt. Mwasaga alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, usalama wa matumizi ya AI, uongozi madhubuti wa data, na ushirikishwaji wa sekta zote katika kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na mapinduzi ya kidijitali.

“Tunapaswa kujenga mfumo wa teknolojia ya AI unaozingatia maadili, usalama, na ushirikishwaji kwa kila Mtanzania,” alisema Dkt. Mwasaga na kuongeza kuwa.

“Ni lazima tushirikiane kama taifa sekta ya umma, binafsi, wataalamu na wanazuoni ili kuhakikisha kizazi cha sasa na vijacho kinanufaika na mapinduzi haya ya teknolojia.”

Mkutano huu umeleta pamoja wataalamu wa teknolojia, watunga sera, wawakilishi wa sekta binafsi, na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili mwelekeo wa AI nchini Tanzania. Aidha, mkutano unalenga kuweka msingi wa sera jumuishi na endelevu zitakazoiwezesha Tanzania kuongoza katika matumizi salama na jumuishi ya teknolojia ya Akili Bandia barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Soft Tech Consultants Africa, Bw. Harish R. Bhatt, akiwasilisha mada katika mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa kuoanisha utawala wa takwimu na maadili ya AI kwa maendeleo endelevu.

“Matumizi ya AI yanapaswa kuongozwa na misingi imara ya kimaadili ili kuhakikisha teknolojia hii inaleta manufaa kwa jamii nzima bila kumwacha mtu nyuma,” alisema Bw. Bhatt, 

Aidha bw. Bhatt alisisitiza juu ya wajibu wa wadau wa teknolojia kuhakikisha kuna uwiano wa uwajibikaji, maadili, na athari chanya kwa jamii.
Naye Mheshimiwa Neema Lugangira, akichangia mijadala ya mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa kutambua si tu fursa bali pia hatari zinazoweza kuambatana na matumizi ya teknolojia ya Akili Bandia (AI).

“Tunapozungumzia fursa, ni lazima pia tuzungumzie hatari. AI si teknolojia isiyoegemea upande wowote, inaweza kutumiwa vibaya. Hivyo basi, uongozi wa kimaadili si hiari bali ni ngao muhimu tunayohitaji,” alieleza kwa msisitizo Mheshimiwa Lugangira.

Ufunguzi wa Tanzania AI Forum 2025 umetajwa kuwa mwanzo thabiti na wa kihistoria katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali unaojengwa juu ya misingi ya maadili, usawa wa kijamii, na uvumbuzi wa kiteknolojia.