Breaking News

MWENEZI WA BAWACHA AJIUNGA CHAUMMA

Dar es salaam - Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Bi. Sigrada Mligo, ametangaza kujiondoa rasmi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akitaja sababu kuu kuwa ni kushindwa kutambuliwa kwa mchango wake na kile alichokiita "unyanyasaji wa ndani ya chama.”

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu katika makao makuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Bi. Mligo alisema kuwa amekuwa akihusishwa kimakosa na migogoro ya ndani ya CHADEMA, jambo ambalo amesema linamvunjia heshima licha ya mchango mkubwa alioutoa kwa chama hicho.

“Mwaka 2019 tuliendesha CHADEMA Digital kwa kusajili wanachama na kushughulikia uchaguzi. Lakini Januari 2025, CHADEMA haikuweza kufanya operesheni kwenye majimbo ya Makete, Wang’ing’ombe na Ludewa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Nilimpigia Katibu Mkuu Mnyika, naye alikiri kuwa bajeti haikuwepo,” alisema Mligo.
Kwa mujibu wake, aliamua kufadhili operesheni hiyo kwa kutumia zaidi ya shilingi milioni 15 kutoka kwa fedha zake binafsi, ili kuhakikisha kuwa majimbo hayo matatu mkoani Njombe yanashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa ndani wa chama.

“Niliigharamia kwa fedha zangu hadi uongozi wa majimbo ukapatikana, ambao baadaye ulipiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa chama. Zote zipo kwenye kumbukumbu, hawawezi kubisha,” aliongeza.
Licha ya kujitolea kwake, Bi. Mligo ameeleza kusikitishwa na kile alichokiita “lugha za kubeza” kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA, ambao alisema wamekuwa wakijinasibisha kuwa “wapambanaji halisi” na kuwadharau wengine.

Kauli ya Bi. Mligo imekuja miezi kadhaa baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa waathirika wa vurugu katika kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, kilichofanyika tarehe 25 Machi 2025 mjini Njombe, ambapo alidai kujeruhiwa na mmoja wa walinzi wa chama hicho.