FERNANDO WOLLE ACHUKUA NA KUREJESHA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KIKABWE KWA TIKETI YA CCM
Kibakwe, Dodoma - Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Fernando Wolle, ametangaza rasmi nia ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Kibakwe, wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, baada ya kuchukua na kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho.
Zoezi hilo limefanyika katika ofisi za CCM wilayani humo, ambapo Ndugu Wolle aliwasili akiwa ameambatana na wafuasi wake pamoja na wanachama wa CCM waliompa sapoti kubwa. Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu, Wolle alieleza dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Kibakwe kwa uaminifu, uwazi na ushirikiano, akisisitiza umuhimu wa maendeleo ya kweli kwa wananchi wote.
“Ninaamini katika siasa safi na uongozi wa kuwatumikia watu. Niko tayari kushirikiana na wananchi wa Kibakwe kuboresha huduma za kijamii, kuinua uchumi na kuendeleza vijana,” alisema Wolle kwa msisitizo.
Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kuteuliwa ndani ya CCM unaendelea kote nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo wagombea wanahimizwa kuzingatia maadili ya chama na kufuata taratibu zote zilizowekwa.
Kwa hatua hii, Ndugu Wolle amejiunga rasmi na orodha ya makada wa CCM wanaowania ridhaa ya chama chao kuwa wagombea rasmi katika uchaguzi wa mwaka huu.





