LAMBECK NYAMBAYA ACHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SEGEREA
Dar es Salaam, Julai 1, 2025 — Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lameck Nyambaya, leo amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Segerea kwa tiketi ya CCM, ikiwa ni hatua ya kuonyesha nia yake ya kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Nyambaya amekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Sylvester Yared, katika ofisi za chama hicho zilizopo wilayani humo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu, Nyambaya amesema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika juhudi zake za kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo katika taifa.
“Nina nia thabiti ya kulihudumia Jimbo la Segerea na kuchangia kwa vitendo juhudi za Rais Samia katika kuwaletea wananchi maendeleo. Niko tayari kushirikiana na wanachama wenzangu wa CCM na wananchi kwa ujumla katika kuhakikisha Segerea inapata maendeleo ya kweli,” alisema Nyambaya.
Nyambaya ameahidi kufanya kampeni za kistaarabu endapo atapitishwa na chama, na kuahidi kushirikiana na wagombea wenzake kuhakikisha CCM inaendelea kushika hatamu ya uongozi wa jimbo hilo.
Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM unaendelea nchi nzima huku wagombea mbalimbali wakiendelea kujitokeza.





