Breaking News

NIT RASMI YAANZA KUTOA KOZI YA URUBANI MWAKA WA MASOMO 2025/26

Dar es salaam - Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeanza rasmi kozi ya mafunzo ya urubani kwa mwaka mpya wa masomo 2025/26 ulioanza mwezi Julai mwaka huu.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Mkufunzi wa Urubani wa NIT, Ashraf Ramadhani, alisema kuwa kozi hiyo mpya imeanza kwa mafanikio na kuwakaribisha wanafunzi kumi, wakiwemo wanawake wanne na wanaume sita.

Ramadhani alieleza kuwa Chuo kimejipanga kikamilifu kuzalisha marubani waliobobea na wataalamu wa anga, jambo ambalo litaleta mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa. Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa gharama nafuu ukilinganisha na awali ambapo wanafunzi walilazimika kusafiri nje ya nchi kupata elimu hiyo kwa gharama kubwa.
“NIT tumejiandaa vizuri, tuna walimu wa kutosha—kwa sasa tuko walimu kumi—na tuna vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia, ikiwemo ndege mpya kwa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wetu,” alisema Ramadhani.

Alifafanua kuwa vigezo vya kujiunga na kozi hiyo ni pamoja na kuwa na umri kuanzia miaka 17, pamoja na afya njema ya macho na akili. Alitoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa ni ya kipekee na yenye manufaa ya muda mrefu.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa NIT, Juma Mandai, aliwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kujiunga na kozi hiyo kwani mbali na kuongeza idadi ya marubani nchini, pia itazalisha ajira lukuki ndani na nje ya nchi.

“Mbali na urubani, NIT pia inatoa mafunzo ya kutengeneza ndege na ufundi wa matengenezo ya ndege. Kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu wa sekta ya anga, na tunaamini kupitia kozi hizi tutachangia kukuza ajira na uchumi wa taifa,” alisema Mandai.

NIT inaendelea kuwa chuo kinachoongoza kwa kutoa mafunzo ya kisasa katika sekta ya usafirishaji, huku sasa kikiwa na mchango mpya katika sekta ya anga nchini Tanzania.