WMA YAWATAKA WANANCHI KUHOJI VIPIMO WANAPOPATA HUDUMA
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa umma wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Bi Veronica Simba akifafanua jambo kuhusu umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa na kutambua kuwa ni haki yao kuuliza kuhusu Vipimo vinavyotumika pindi wapatiwapo huduma.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Temeke (WMA) Bwana Hilolimus Mahundi akielezea faida za matumizi ya vipimo hususani vilivyohakikiwa na WMA mapema leo Julai 11, 2025 katika banda lao maonyesho ya 49 ya sabasaba jijini dar es salaam.
Dar es Salaam, Julai 11, 2025 — Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Bi. Veronica Simba, ametoa wito kwa wananchi kutumia haki yao ya kuuliza na kujiridhisha kuhusu vipimo vinavyotumika wakati wa kupata huduma kutoka kwa wafanyabiashara katika sekta mbalimbali.
Akizungumza kwenye Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Bi. Simba alisema ni muhimu kwa wananchi kuwa na uelewa na uthubutu wa kuuliza endapo vipimo vilivyotumika vimehakikiwa rasmi na Serikali kupitia WMA.
“Kuuliza ni haki ya kila mwananchi. Siyo hisani,” alisema. “Kwa mfano, ukienda bucha ukapimiwa nyama, una haki ya kumuuliza muuzaji kama mzani wake umehakikiwa. Uthibitisho wa hili upo kwenye stika ya Wakala wa Vipimo.”
Bi. Simba alisema licha ya wananchi wengi kuwa na uelewa kuhusu vipimo, bado wengi hukosa ujasiri wa kuuliza ili kuhakikisha hawapunjwi. Alisisitiza kuwa WMA ipo kwa ajili ya kuhakikisha haki ya mlaji inalindwa na kila kipimo kinachotumika kinakuwa sahihi.
Kwa mujibu wa Bi. Simba, WMA imekuwa ikishiriki maonyesho ya Sabasaba tangu yalipoanza Juni 28, na hadi sasa wamehudumia wananchi wengi waliotembelea banda lao na kujifunza kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi katika huduma na bidhaa.
“Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kila kipimo kinachotumika kwenye huduma au bidhaa mbalimbali kimehakikiwa ili kumlinda mlaji,” alisema. “Tunafanya kazi katika sekta zote zinazohusiana na vipimo, kuanzia biashara, kilimo, afya hadi usafirishaji.”
Aliendelea kufafanua kuwa bidhaa nyingi kwenye maduka makubwa kama mafuta, kahawa au sukari zinaonyesha vipimo kama "lita moja" au "nusu kilo", lakini ni jukumu la WMA kuhakikisha kuwa kile kilichoandikwa ndicho kilichopo.
Aidha, alisema WMA inahakikisha mizani inayotumika katika maduka ya nyama imehakikiwa, na kuthibitishwa kwa kuweka stika maalum ya Wakala.
Katika sekta ya kilimo, Bi. Simba alisema WMA inahakiki vipimo vya mazao ya kimkakati kama korosho na pamba, huku kwenye sekta ya afya wakihakikisha mizani zinazotumika kupimia uzito wa wagonjwa hospitalini ni sahihi, kwani matibabu hutolewa kulingana na vipimo hivyo.
Bi. Simba pia alieleza kuwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye maonyesho ya Sabasaba, WMA imebaini kuwa elimu kuhusu vipimo ni ya msingi na inapaswa kusambazwa zaidi. Alitaja mpango wa kuanzisha klabu za vipimo mashuleni, kwa kushirikiana na walimu, ili kuwaelimisha watoto kuhusu kazi na umuhimu wa Wakala wa Vipimo.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Temeke, Bw. Hilolimus Mahundi, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanapimiwa gesi ya kupikia kwa kutumia mizani iliyohakikiwa na WMA.
“Ukichukua mtungi wa gesi, hakikisha umepimwa na upo sahihi kabla ya kuondoka nao. Kama kuna shaka, wasiliana na ofisi ya WMA iliyoko katika kila mkoa kwa msaada wa kisheria,” alisema Bw. Mahundi.
WMA imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kulinda haki ya mlaji kwa kuhakikisha kuwa kila kipimo kinachotumika katika huduma na bidhaa mbalimbali ni sahihi na kimeidhinishwa na Serikali.







