Breaking News

ROBOTI SASA KUFIKIRI NA KUFANYA KAZI KWA NIABA YA MTUMIAJI - CHATGPT YAZINDUA “AGENT MODE”

Kampuni ya OpenAI imetangaza kuzindua kipengele kipya katika akili mnemba yake ya ChatGPT kitakachomruhusu roboti huyo kutekeleza baadhi ya majukumu kwa niaba ya mtumiaji. Kipengele hicho kipya, kilichopewa jina la “Agent Mode”, ni sehemu ya mapinduzi makubwa ya kiteknolojia yanayolenga kubadili namna watumiaji wanavyopata na kutumia taarifa mitandaoni.

Kupitia “Agent Mode”, ChatGPT itaweza kufanya kazi nyingi ambazo hapo awali zilihitaji mtumiaji kuhama kutoka programu moja hadi nyingine. Badala yake, akili hiyo mnemba itaweza kuchakata taarifa, kufikiri, na kutekeleza maagizo kwa njia ya kiotomatiki kupitia mfumo wake wa kompyuta ya kidijitali (virtual computer).

Kwa mujibu wa OpenAI, ChatGPT sasa itaweza kusaidia katika majukumu kama vile:

- Kukagua kalenda na kutoa taarifa kuhusu matukio yajayo

- Kutoa mapendekezo ya viungo vya chakula kulingana na aina ya mlo

- Kushauri aina ya mavazi ya kuvaa kwa hafla mbalimbali kama harusi, ibada au tafrija

Katika video ya maelezo iliyotolewa na OpenAI, mtumiaji mmoja aliomba ushauri wa mavazi kwa ajili ya harusi katika mazingira tofauti — kanisani, hotelini na ukumbini — ambapo ChatGPT ilitoa mapendekezo ya mavazi matano kulingana na hali ya tukio, na mtindo wa mtumiaji.

Kipengele hiki cha “Agent Mode” kinapatikana kwa watumiaji wa huduma za kulipia pekee, zikiwemo ChatGPT Pro, Plus, na Team Plan.

HATARI ZA TAARIFA ZA FARAGHA

Hata hivyo, OpenAI imeonya kuwa pamoja na uwezo wake mpya, ChatGPT haipaswi kupewa taarifa binafsi au nyeti kama nambari za benki, nywila, au taarifa nyingine za faragha. Pia, haitaruhusiwa kufikia huduma kama barua pepe binafsi au kutekeleza majukumu yenye hatari ya kiusalama kama vile miamala ya kifedha, bila uangalizi wa karibu wa mtumiaji.

OpenAI imeeleza kuwa licha ya maendeleo haya, usalama wa watumiaji na matumizi ya maadili ya teknolojia utaendelea kupewa kipaumbele.