Breaking News

SHEIKH MOHAMMED ABDI AONGOZA ZOEZI LA KUFANYA USAFI


Kigogo, Dar es Salaam – Katika kuadhimisha mwezi mtukufu wa Muharram 1447 Hijria, waumini wa madhehebu ya Shia wameungana kwa shughuli ya kijamii ya usafi wa mazingira, wakilenga kumuenzi Swahaba na Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Imam Hussein (a.s), aliyeuawa kishujaa katika ardhi ya Karbalaa, Iraq.

Zoezi hilo la usafi lililopewa kaulimbiu ya mwaka huu "Karbalaa Siri ya Ushindi Wetu", lilifanyika kuanzia eneo la Kigogo Mbuyuni hadi Kigogo Mwisho, likiwa na lengo la kutekeleza kauli ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) isemayo “Usafi ni katika Imani.”
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Samahat Sheikh Mohamed Abdi, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shia Tanzania Ithna-Asheri Community (TIC) na Naibu Mudir wa Hawzat Imam Swadiq (a.s), alisisitiza kuwa tukio hilo sio tu ni ibada bali pia ni njia ya kudhihirisha maadili ya Kiislamu katika jamii.

“Tunafanya haya kila mwaka kama njia ya kuuenzi ujasiri, uadilifu, na kujitolea kwa Imam Hussein (a.s), pamoja na kutekeleza mafundisho ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) kuhusu usafi wa mwili na mazingira kama sehemu ya imani,” alisema Sheikh Mohamed.
Shughuli hiyo ilijumuisha waumini wa rika zote, huku ikilenga kujenga mshikamano wa kijamii, kukuza usafi wa kimazingira na kiroho, na kuendeleza mapambano dhidi ya dhulma, kwa kuiga msimamo wa Karbalaa.

Wakazi wa maeneo husika waliipongeza jamii hiyo kwa juhudi zao za kutunza mazingira na kuonyesha mfano wa kuigwa katika kushirikiana na jamii kwa vitendo vyenye tija.

Tukio hilo limechochea ari ya mshikamano wa kidini na kijamii, likionyesha kuwa mapambano ya Karbalaa yanaendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya hadi leo.