Breaking News

VETA WABUNI MASHINE YA KUTENGENEZA CHAKULA BORA CHA MIFUGO

Dar es Salaam — Chuo Cha Ufundi Stadi (VETA) Songea kimebuni mashine maalum ya kutengeneza chakula cha mifugo aina ya pelet, ambayo inatarajiwa kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula bora kwa ajili ya mifugo.

Akizungumza katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, Mkufunzi wa fani ya Uundaji na Uungaji vyuma kutoka VETA Songea, Bw. Sussack Mbulu, alisema mashine hiyo ni matokeo ya ubunifu wa wanafunzi wa chuo hicho kwa kushirikiana na walimu wao.

"Hapa kwenye banda la VETA Songea tuna bidhaa na mashine ambazo ni bunifu zetu, zimetokana na kazi halisi zilizofanywa na wanafunzi wetu kwa viwango vya hali ya juu," alisema Bw. Mbulu.
Aidha, alibainisha kuwa mashine hiyo ya Pelet imelenga kurahisisha upatikanaji wa chakula bora cha mifugo kwa gharama nafuu, huku ikipunguza matumizi yasiyo sahihi ya kemikali na kuongeza usalama wa vyakula vya mifugo. Chakula kinachozalishwa hupatikana katika mfumo wa punje punje (chenga chenga), unaorahisisha ulaji na mmeng'enyo kwa mifugo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya maonyesho ya Sabasaba ni "Fahari ya Tanzania" ikilenga kuonesha ubunifu, ujasiriamali na maendeleo ya viwanda vya ndani. VETA Songea ni miongoni mwa taasisi zilizovutia wageni wengi kwa ubunifu wao wa kiteknolojia unaolenga kuboresha maisha ya wananchi kupitia elimu ya ufundi.