WMA YATOA ELIMU KWA WANUNUZI WA MAFUTA, YASISIZA UMAKINI WANAPOKUWA KATIKA VITUO VYA MAFUTA
Dar es Salaam, Julai 4, 2025 — Wakala wa Vipimo (WMA) umetoa elimu na ushauri kwa wananchi wanaonunua mafuta katika vituo mbalimbali nchini, ukiwa ni mkakati wa kuhakikisha haki za walaji zinalindwa.
Akizungumza katika kipindi cha KISS RIPOTI kilichorushwa na redio ya Kiss FM leo Julai 4, 2025, Meneja wa Kitengo cha Bandari kutoka WMA, Alfred Shungu, aliwahimiza wananchi kuwa makini wanapohudumiwa katika vituo vya mafuta.
“Mteja akihisi amepunjwa wakati wa kununua mafuta, anatakiwa kutoa taarifa kwa kupiga namba ya bure 0800110097, ili Wakala wa Vipimo iweze kufuatilia na kuchukua hatua stahiki,” alieleza Shungu.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanapata risiti baada ya kulipia mafuta, kama sehemu ya uthibitisho wa huduma waliyopewa
Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa WMA, Bi Veronica Simba, alibainisha kuwa Wakala umeendelea kutumia njia mbalimbali kuelimisha umma kuhusu majukumu yake, ikiwa ni pamoja na vipindi vya redio, televisheni, mitandao ya kijamii, na mikutano ya moja kwa moja na wananchi.
“Tunafanya juhudi kuhakikisha kila mwananchi anafahamu haki yake na jinsi ya kushirikiana na Wakala wa Vipimo kulinda haki hizo, hasa kwenye bidhaa nyeti kama mafuta,” alisema Bi Veronica.
Wakala wa Vipimo (WMA) ni taasisi ya Serikali inayohakikisha kuwa vipimo vinavyotumika katika biashara mbalimbali, vimekaguliwa na vimeidhinishwa kwa mujibu wa sheria, ili kumlinda mlaji dhidi ya udanganyifu.





