Breaking News

EWURA YAHAMASISHA WANANCHI KUHUSU MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Arusha – Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi kupitia banda lake katika Maonyesho ya 31 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi Njiro, jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa EWURA, Mhandisi Lorivii Long’idu, alisema kuwa maonyesho hayo ni fursa muhimu ya kuelimisha umma kuhusu majukumu ya EWURA, yakiwemo upangaji wa bei za mafuta kote nchini pamoja na usimamizi wa huduma za nishati na maji kwa mujibu wa sheria.

Mhandisi Long’idu alieleza kuwa moja ya malengo makuu ya EWURA ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka 10 wa Serikali unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 30 ya Watanzania watakuwa wamehamia kutoka matumizi ya nishati isiyo salama na kuanza kutumia nishati safi kama gesi.

“Tunatumia fursa hii kusisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni muhimu si tu kwa afya ya jamii, bali pia kwa ajili ya kulinda mazingira,” alisema. Aliongeza kuwa tafiti za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa magonjwa mengi ya mfumo wa upumuaji yanatokana na matumizi ya kuni na mkaa majumbani.
Kwa upande mwingine, Mhandisi Long’idu alibainisha kuwa EWURA inaendelea kusimamia kwa karibu usambazaji wa gesi ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata gesi yenye ujazo sahihi kama inavyopaswa kupimwa. Alisema tayari baadhi ya mawakala wa gesi wamekamatwa kwa kukiuka sheria, na kesi zao zipo mahakamani zikisubiri uamuzi.

“Ni jukumu la kila msambazaji mkubwa kuhakikisha wauzaji wadogo wanafuata sheria zote. Wananchi nao wanapaswa kuhakikisha kuwa gesi wanayonunua imepimwa na imejaa kikamilifu,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wananchi kutembelea banda la EWURA katika maonyesho hayo ili kupata elimu ya kina kuhusu huduma za nishati na maji, pamoja na kuwasilisha changamoto zinazowakabili kuhusu umeme, maji, mafuta na gesi, ili zipatiwe ufumbuzi stahiki.