MKUU WA CHUO CHA NIT ATEMBELEA WADAU MAONESHO YA NANENANE 2025
Dodoma — Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya, ametembelea mabanda ya wadau mbalimbali katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya maonesho jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mgaya alipata fursa ya kujionea shughuli na huduma zinazotolewa na taasisi zinazohusiana na sekta ya usafirishaji, ambazo ni washirika wakuu wa maendeleo katika sekta hiyo muhimu nchini. Miongoni mwa mabanda aliyotembelea ni ya Mamlaka ya Usafiri Ardhini (LATRA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA-CCC), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Air Tanzania, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), pamoja na Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC).
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Dkt. Mgaya aliwapongeza wadau hao kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha sekta ya usafirishaji nchini, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya NIT na taasisi hizo ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya taaluma, utafiti na teknolojia katika sekta hiyo. Aidha, alieleza kufurahishwa na namna taasisi hizo zinavyotoa huduma bunifu zinazochangia pia katika sekta nyingine kama kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Sekta ya usafirishaji ni kiungo muhimu kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa sekta nyingine. Ushirikiano wetu na taasisi hizi utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha tunawajengea vijana uwezo wa kitaaluma na kiutendaji,” alisema Dkt. Mgaya.
Maonesho ya NaneNane ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi 2025”, na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 8 Agosti 2025.









