SHEIKH JALALA AONGOZA MATEMBEZI YA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W.)
Dar es salaam - Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithna Asharia nchini Tanzania leo (22 Agosti 2025) wamefanya matembezi ya amani kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mtume Muhammad (S.A.W.W.).
Matembezi hayo yalianzia Ilala Boma na kuishia katika Masjidil-Ghadeer Kigogo Post, ambapo yaliongozwa na Sheikh Hemedi Jalala. Akizungumza baada ya matembezi hayo, Sheikh Jalala alisema siku hiyo ni ya majonzi lakini pia ya kuenzi na kukumbuka maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W.W.) pamoja na mafundisho yake.
"Leo tumetoka barabarani kufanya matembezi ya amani kukumbuka kifo cha Mtume Muhammad (S.A.W.W.), kwa kuendelea kuyaishi yale aliyoyasisitiza katika kipindi chote cha uhai wake," alisema Sheikh Jalala.
Ameongeza kuwa kumbukumbu hiyo iwe chachu ya kudumisha amani, mshikamano na umoja si tu miongoni mwa Waislamu wa madhehebu yote, bali pia kati yao na wasio Waislamu, kwa kuwa hayo ndiyo yalikuwa maisha na mafundisho ya Mtume (S.A.W.W.).
Katika ujumbe wake kwa taifa, Sheikh Jalala alitoa rai kwa Watanzania kuelekea uchaguzi mkuu ujao kudumisha amani na utulivu uliopo nchini kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
"Katika kipindi hiki tunachoelekea uchaguzi mkuu, Watanzania tuendelee kuenzi mshikamano na amani tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu, kwani ni tunu ya kipekee," alisema Sheikh Jalala.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake, ili waendelee kuongoza kwa hekima huku Mwenyezi Mungu akiwalinda na mabaya, hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.