Breaking News

“AHADI ZA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA: AFYA BURE, BIMA KWA WOTE NA AJIRA MPYA”

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga kutekeleza mpango wa siku 100 wenye kuzingatia sekta za afya, elimu, ajira na ujasiriamali, ikiwa ni sehemu ya malengo ya kujenga usawa wa kijamii na kuimarisha huduma muhimu kwa wananchi.

Matibabu Bila Malipo kwa Wasiojiweza

Katika utekelezaji wa mpango huu, serikali imeahidi kugharamia kwa asilimia 100 matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wa kipato cha chini, hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama saratani, figo, moyo, kisukari, mifupa na mishipa ya fahamu.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025, Tanzania yenye watu milioni 65, inakadiriwa kuwa na wananchi milioni 17.16 (sawa na asilimia 26.4) wanaoishi chini ya kiwango cha umasikini wa kipato. Hawa ndio wanaolengwa moja kwa moja na mpango huu wa matibabu bila malipo.

Bima ya Afya kwa Wote

Serikali pia imeweka kipaumbele kuanzisha rasmi Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, ukilenga makundi maalum kama wazee, mama wajawazito, watoto na watu wenye ulemavu. Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 zinaonyesha kuwa kati ya Watanzania milioni 61.7, zaidi ya asilimia 65.1 wanaishi vijijini ambako changamoto ya upatikanaji wa huduma bora za afya bado ni kubwa.

Licha ya umuhimu wake, ni asilimia 7 pekee ya Watanzania waliokuwa na bima ya afya kufikia mwaka 2022, hali iliyodhihirisha pengo kubwa la upatikanaji wa huduma.

Ajira Mpya 5,000 Sekta ya Afya

Kupitia ahadi za siku 100, serikali inatarajia kuajiri wahudumu wa afya wapya 5,000 wakiwemo wauguzi na wakunga. Hatua hii inalenga kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto na kupunguza mzigo wa kazi kwa wahudumu waliopo.

Kwa sasa Tanzania ina jumla ya wahudumu wa afya wapatao 137,000 na uwiano wa mtoa huduma mmoja kwa wagonjwa 474. Ajira mpya zitaongeza idadi ya wahudumu hadi takriban 142,000 na kupunguza uwiano huo hadi 1:458. Kiwango hicho kinaisogeza Tanzania karibu zaidi na lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO) la 1:439, na kuongeza ufanisi wa huduma kutoka asilimia 92.6 hadi 95.2 ya lengo hilo.

Bilioni 200 kwa Biashara Ndogo

Katika sekta ya ujasiriamali, serikali imetenga shilingi bilioni 200 kusaidia biashara ndogo ndogo na vijana. Kiwango hiki kinatarajiwa kuanzisha biashara mpya takribani 400,000 kwa mtaji wa awali wa shilingi 500,000 kila moja.

Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), zaidi ya asilimia 71.7 ya vijana wenye umri kati ya miaka 25–29 barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hufanya kazi zisizo rasmi. Hatua ya serikali kuwezesha mitaji ni muhimu katika kukuza ajira, ubunifu na mchango wa vijana kwenye uchumi.

Ajira za Walimu 7,000 wa Sayansi

Katika sekta ya elimu, Rais Samia ameahidi ajira mpya za walimu wa sayansi 7,000 ili kupunguza pengo la walimu kwa wanafunzi. Kwa sasa Tanzania ina jumla ya wanafunzi zaidi ya milioni 15 kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, huku ongezeko kubwa la wanafunzi likichochewa na utekelezaji wa elimu bila malipo.

Uwiano wa walimu kwa wanafunzi ni 1:163 kwa awali, 1:49 kwa msingi na 1:27 kwa sekondari – viwango ambavyo ni juu ya mapendekezo ya UNESCO ya 1:25 kwa awali, 1:40 kwa msingi na 1:25 kwa sekondari. Ajira hizi mpya zitaboresha zaidi uwiano huo na kuimarisha ubora wa elimu ya sayansi na hisabati, ikionyesha uelekeo wa Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.