Breaking News

CHAMA CHA NLD CHAHITIMISHA KAMPENI KASKAZINI, SASA KUELEKEA KANDA YA ZIWA

Chama cha NLD kimekamilisha awamu ya kampeni zake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Tanga, Babati na Arusha, ambapo kimefanikiwa kufanya zaidi ya mikutano 45 ya kampeni kwa mfumo wa kijiji kwa kijiji na kata kwa kata.

Kampeni hizo zimefanyika kwa mtindo wa mobile kampeni, ambapo Mgombea Urais wa chama hicho amekuwa akiwafuata wananchi walipo, huku timu ya kampeni ikiendelea na mikakati ya nyumba kwa nyumba mara baada ya mgombea kuhamia wilaya nyingine.

Mgombea huyo amefika katika maeneo ya pembezoni kama Jasini, Mkinga, Msomela, Handeni na Mlalo wilayani Lushoto, hatua ambayo chama kimesema inawapambanua na wagombea wengine waliobaki mijini. Kwa mujibu wa tathmini ya chama, wananchi wengi wanapenda kuthaminiwa na kufuatwa majumbani kwao, jambo linalowapa nafasi ya kumsikiliza kwa makini na kuelewa sera pamoja na ilani ya NLD.

Kupitia mkakati huo wa kampeni shirikishi, NLD inajipambanua kama chama kinachojali kada zote za wananchi bila kujali umbali wa maeneo wanayoishi. Tathmini pia zinaonyesha kuwa kati ya wagombea 16 wa urais, mgombea wa NLD, Mhe. Doyo, ni miongoni mwa wachache walioweza kuwafikia wananchi moja kwa moja vijijini.

Baada ya mafanikio ya Kaskazini, chama hicho sasa kimeelekeza nguvu zake katika Kanda ya Ziwa, likiwemo mikoa ya Mara, Mwanza, Geita na Bukoba, kwa lengo la kuendeleza kampeni za ukaribu na wananchi na kusikiliza changamoto zao moja kwa moja.