Breaking News

TBS YAONDOA SOKONI TANI 42 ZA VYAKULA VYA WATOTO VYENYE MIDOLI

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi akielezea mafanikio ya TBS katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa Habari jijini dar es salaam 

Dar es Salaam – Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeondoa sokoni jumla ya tani 42 za bidhaa za chakula cha watoto maarufu zilizokuwa zikisambazwa zikiwa na midoli ndani yake.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa TBS, Kandida Shirima, amesema hatua hiyo imefuata baada ya uchunguzi kubaini kuwepo kwa viwanda vilivyokuwa vikizalisha na kusambaza bidhaa hizo kinyume cha sheria.

Akizungumza katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari jana, kuelezea mafanikio ya TBS katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Shirima alisema baadhi ya wazalishaji walikuwa wakifunga vyakula na midoli kwa lengo la kuvutia watoto na watumiaji, jambo lililo hatarisha usalama wa walaji.

“Tulichukua hatua ya kutoa taarifa kwa umma na kuvifikia viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo kisha kusitisha uzalishaji wake. Tumefanya ukaguzi kupitia ofisi zetu za kanda nchi nzima na tumeziondoa sokoni tani 42. Hadi sasa hakuna tena anayezalisha bidhaa hizo,” alisema Shirima.

TBS imesisitiza itaendelea kusimamia viwango na kuzuia bidhaa hatarishi kuingia sokoni ili kulinda afya na usalama wa watumiaji.