CHINI YA UONGOZI WA RAIS SAMIA: AONGOZA MAGEUZI YA VIWANDA, KONGANI KUBWA KUJENGA UWEKEZAJI NA AJIRA MPYA NCHINI
Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeanzisha kongani mbalimbali za viwanda nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi wa viwanda na kuvutia wawekezaji.
Miongoni mwa miradi hiyo ni Modern Industrial Park iliyopo Mlandizi, mkoani Pwani. Ujenzi wa kongani hiyo ulianza Septemba 2021 na unatarajiwa kugharimu shilingi trilioni 3.5. Eneo hilo lina ukubwa wa ekari 1,077 na limegawanywa katika viwanja 210, vikiwemo 202 vya viwanda, viwili vya vituo vya umeme vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 54 na 400, viwili vya biashara, vitatu kwa huduma za jamii na kimoja cha bandari kavu.
Kongani nyingine ni TAMCO Industrial Park iliyopo Kibaha mkoani Pwani chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC). Eneo hili lina ukubwa wa ekari 201.63 na litajumuisha viwanda vya dawa, magari, nguo na vinginevyo. Hadi kufikia Mei 2025, tayari wawekezaji 14 wamesaini mikataba saba ya kuwekeza katika eneo hilo.
Aidha, Serikali imeanzisha Kwala Industrial Park lenye ukubwa wa ekari 2,500, ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi imehusisha ekari 500. Baadhi ya viwanda tayari vimeanza kujengwa na kongani hiyo inatarajiwa kuwa na viwanda vikubwa 200 na vidogo 300 pindi ujenzi utakapokamilika. Mradi huu unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 100,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 500,000, sambamba na kuzalisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 6 za Marekani.
Mwekezaji mkuu wa mradi huo, kampuni ya Sino Tan, inatarajia kukamilisha ujenzi wote ifikapo mwaka 2027. Kwala Industrial Park pia itahusisha bandari kavu na huduma za reli ya kisasa (SGR) kutoka Kwala hadi Dodoma kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo.




