JESHI LA POLISI KUFANYA UCHUNGUZI WA VIFO VYA WATU WAWILI DAR
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linafanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya watu wawili lililotokea Septemba 25, 2025 katika eneo la Taliani, Chanika, wilayani Ilala.
Waliopoteza maisha wametajwa kuwa ni Mashua Bakari Mashua (35) na Salha Yusuph Halfan (22), wote wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, miili ya marehemu hao ilikutwa ndani ya chumba cha kupanga alichokuwa akiishi marehemu Salha, ikiwa na majeraha makubwa yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali. Inadaiwa kuwa mwanaume alimjeruhi mwanamke na baadaye kujijeruhi mwenyewe, hali iliyopelekea wote kupoteza maisha.
Taarifa hiyo ya polisi imeeleza kuwa chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni wivu wa mapenzi na mzozo ulioibuka kati ya wawili hao.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.





