Breaking News

NGORONGORO YANADI FURSA ZA UWEKEZAJI NA UTALII KATIKA MAONESHO YA "MY TANZANIA ROADSHOW 2025

Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Huduma za Shirika Ngorongoro, Bw. Aidan Makalla, ameongoza msafara wa Shirika hilo kushiriki katika Maonesho ya “My Tanzania Roadshow 2025 Europe” yanayofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 27 Septemba 2025 katika miji ya Stuttgart (Ujerumani), Salzburg (Austria), Ljubljana (Slovenia) na Milan (Italia).

Bw. Makalla, akiwa ameambatana na Bw. Abdiel Laizer, Afisa Utalii Mkuu Msaidizi, amekutana na mawakala mbalimbali wa utalii kwa lengo la kunadi vivutio vya kipekee vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii.
Maonesho haya, yanayoandaliwa na Kampuni ya KILIFAIR, ni jukwaa mahsusi la kutangaza vivutio vya utalii na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha utalii barani Ulaya. Zaidi ya kampuni 80 kutoka Tanzania na Ujerumani zinashiriki katika maonesho haya, yakitoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kukuza mtandao wa masoko ya utalii.

Shirika la Hifadhi ya Ngorongoro linasisitiza dhamira yake ya kuendelea kutangaza vivutio vyake vya kipekee duniani, ikiwemo Krateta ya Ngorongoro, Hifadhi za Wanyamapori na Urithi wa Dunia wa UNESCO, ili kuongeza idadi ya watalii na kuvutia wawekezaji wa kimataifa.