KUPATWA KWA MWEZI KUKIONEKANA KESHO NCHINI TANZANIA
Dar es Salaam, Septemba 6, 2025 – Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa kutakuwa na tukio la kupatwa kwa Mwezi usiku wa kesho, Septemba 7, 2025, ambalo litaonekana katika maeneo mbalimbali ya dunia ikiwemo hapa nchini.
Kwa mujibu wa TMA, tukio hilo litahusisha kupatwa kwa Mwezi Sehemu na pia Kupatwa Kikamilifu. Hapa nchini, kupatwa kwa sehemu ya Mwezi kunatarajiwa kuanza mara tu baada ya jua kutua na kuendelea hadi saa 2:29 usiku. Baada ya hapo, kupatwa kikamilifu kutaanza kuonekana kuanzia saa 2:30 usiku hadi saa 3:52 usiku, na hatimaye kupatwa kwa sehemu kuhitimisha tukio hilo kuanzia saa 3:53 hadi saa 5:55 usiku. Kwa ujumla, tukio lote litadumu kwa takribani saa sita.
Wataalamu wa hali ya hewa wamesema kuwa tukio hilo halitatarajiwa kuleta madhara yoyote, ingawa lina uhusiano wa moja kwa moja na mzunguko wa mwezi unaochangia kupwa na kujaa kwa maji baharini. Katika kipindi hicho, kina cha maji baharini kinatarajiwa kuongezeka, lakini hakutakuwa na athari kubwa.
Aidha, TMA imesema hali ya anga inatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, hivyo kutatoa fursa nzuri kwa wananchi kushuhudia tukio hilo kwa macho.
Mamlaka ya Hali ya Hewa imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia kwa ukaribu tukio hilo na kutoa taarifa zaidi endapo kutahitajika.