SHEIKH JALALA: TUISHI MAFUNDISHO YA MTUME MUHAMMAD S.A.W.W KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO
Dar es Salaam – Kiongozi Mkuu wa Waislamu wa Jumuiya ya Shia Ithna’ashariyyah Tanzania, Sheikh Hemedi Jalala, amewataka Waislamu na wananchi kwa ujumla kuenzi na kuishi mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), akisisitiza amani, upendo na mshikamano kama nguzo kuu za maisha.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maulid na tukio la upandishaji wa bendera ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) lililofanyika leo katika Masjid Ghadiir, Kigogo Post jijini Dar es Salaam, Sheikh Jalala alisema tukio hilo ni alama ya kumbukumbu na mwongozo wa kuishi maisha yenye mshikamano bila ubaguzi wa kiimani.
“Mtume Muhammad (s.a.w.w) alitufundisha mshikamano na upendo bila kujali tofauti za madhehebu au dini. Tunaposherekea kuzaliwa kwake, tunapaswa kuenzi mafundisho yake kwa vitendo,” alisema Sheikh Jalala.
Katika hotuba yake, alitumia nafasi hiyo pia kuliombea taifa na kuwataka Watanzania kudumisha amani na mshikamano hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa urais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
“Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kuendeleza amani tuliyonayo na awajalie viongozi wetu, wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hekima na ulinzi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu,” aliongeza Sheikh Jalala.
Maadhimisho ya Maulid ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) yatafanyika rasmi Septemba 10, 2025 katika viwanja vya Pipo, Kigogo Post, jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.