MGOMBEA URAIS CUF ATAKA AMANI, AAHIDI MABADILIKO MAKUBWA
Na Woinde Shizza, Arusha - Mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Samandito Gombo ameendelea na kampeni zake jijini Arusha, akifanya mkutano mkubwa katika eneo la Morombo ambapo amewataka wananchi kulinda amani na mshikamano wa taifa, huku akihimiza wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu.
Akihutubia umati wa wafuasi na wananchi wa eneo hilo, mgombea huyo alisema kura za wananchi ni chachu ya mabadiliko na maendeleo ya kweli, akisisitiza kuwa taifa linahitaji viongozi wapya wenye maono mapya ya kuwaletea wananchi nafuu ya maisha.
“Mimi nawaomba Watanzania wenzangu, tuendelee kulinda amani ya nchi yetu, amani ni nguzo ya maendeleo, na ninawaomba mkanichague ili kwa pamoja tulete mabadiliko makubwa yatakayogusa kila sekta ya maisha,” alisema.
Aliahidi kusimamia uchumi kwa kupunguza gharama za maisha, kupambana na mfumuko wa bei na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za taifa, Vilevile, alisema kilimo kitawekwa kipaumbele ili wakulima wapate pembejeo kwa gharama nafuu na masoko ya uhakika.
Kwa upande wa sekta ya elimu, mgombea huyo alisema serikali itakayoundwa na CUF itaongeza bajeti ya elimu, kuajiri walimu wapya, kuboresha miundombinu ya shule na kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi, hususani wale wa maeneo ya vijijini.
Naye mgombea ubunge wa chama hicho, Zuberi Mwinyi, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wampe ridhaa ya kuwaongoza bungeni, akiahidi kushirikiana nao kuleta maendeleo ya haraka katika jimbo lao.
Alisema endapo atachaguliwa, ataweka nguvu katika kupanua fursa za ajira kwa vijana, kuboresha huduma za afya, kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.
“Sitawaangusha wananchi wa jimbo hili, nitahakikisha tunashirikiana kuondoa changamoto zinazowakabili kila siku na kuharakisha maendeleo kwa manufaa ya wote,” alisema Mwinyi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho na wafuasi kutoka maeneo tofauti ya Arusha, ambapo wote walisisitiza mshikamano na mshikikiano kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29.





