MWENYEKITI WA NEC AKAGUA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU MKOANI MBEYA
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mheshimiwa Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, Septemba 19, 2025 ametembelea Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika Majimbo ya Uchaguzi ya Mbeya Mjini na Uyole, ambapo amepokea taarifa ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wasimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya.
Katika ziara hiyo, Jaji Mwambegele amekagua vifaa mbalimbali vya Uchaguzi ambavyo tayari vimepokelewa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Aidha, alipata fursa ya kutembelea kampeni za wagombea Ubunge wa vyama vya CUF na CCM katika majimbo hayo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Tume, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inawakumbusha wananchi kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi huo kwa kauli mbiu isemayo: "Kura Yako Haki Yako – Jitokeze Kupiga Kura."











