WAMACHINGA WAFUNGUKA JINSI VURUGU ZILIVYOWAUMIZA KIUCHUMI
Vurugu na machafuko yaliyojitokeza kufuatia Oktoba 29, siku ya kupiga kura, yameelezwa kusababisha athari kubwa ya kiuchumi na kisaikolojia kwa wafanyabiashara wadogo, maarufu kama Wamachinga, katika Soko la Kariakoo.
Wawakilishi wa wafanyabiashara hao wametoa wito kwa Watanzania kutumia fursa ya mazungumzo badala ya ghasia, wakisisitiza kuwa wananchi wa chini ndio wanaoishia kuumia zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, Jabir Makunbga, mjumbe wa Taasisi ya Wamachiunga Kariakoo (KAWASO), alieleza kwamba machafuko hayo yameleta athari kubwa kiuchumi, kimawazo, na kuunda hofu kubwa kwa wafanyabiashara.
"Tangu kuanza kwa fujo Oktoba 29, familia zao na wao wenyewe wameteseka sana," alisema Bw. Makunbga.
Aliongeza kuwa Wamachinga wengi hutegemea kufika sokoni kuhangaika kila siku ili kurejesha kipato jioni kwa ajili ya familia zao. Alitaka wananchi watumie fursa ya kuzungumza matatizo badala ya kufanya ghasia, huku akitaka viongozi wahakikishe wanawasikiliza wananchi kwa kuwa sote ni watu wa taifa moja na tunategemeana.
Kwa upande wake, Eliezer Wilson, mjumbe wa Kamati tendaji ya Taasisi ya Wamachinga Kariakoo KAWASO, amefafanua zaidi athari hizo na kutoa wito mzito kwa viongozi wa kisiasa.
"Tunawataka wanasiasa kuzungumza na kuacha kutunishiana misuli kwa kuwa wanaokuja kuumia sio wanasiasa, bali wananchi wa chini," Bw. Wilson alisema.
Amesisitiza kuwa mtawala anapotoa nafasi ya mazungumzo, waendelee kuzungumza na sio kuamsha fujo. Ameonya wanasiasa wasikurupuke kwa kuiga wala kushawishi watu kufanya ghasia, akieleza kuwa hatima yake ni nzito kwa taifa.
Bw. Wilson alieleza kuwa tangu aanze maisha ya biashara ndogo ndogo hajawahi kushuhudia shida kama iliyotokea sasa.
"Watanzania wengi wanaishi kama ndege; asubuhi wanaenda kutafuta warejeshe chakula jioni. Kitendo cha ghafla kuwa katika vizuizi vya kutotembea na kulala mapema ni shida," alisema.
Naye Fadhili Mwango, Machinga wa Kariakoo na Narung'ombe, alikiri kuathirika sana na vurugu zilizoibuka. Alisisitiza kuwa vurugu hizo zimezua balaa la kupanda kwa bei na kukosekana kwa mahitaji sokoni.
Bw. Mwango alitoa wito kwa vijana wenzake, ambao wengi ndio walioshiriki, kuachana na kusukumwa na mambo wasiyoyajua.
"Wengi wakiulizwa hata hawajui nini wanakitaka, ila tu kushiriki. Wamekuwa wakifuata mkumbo," alieleza, akiongeza kuwa kitendo hicho kimesababisha hasara kwa taifa, wazazi wao, na familia zao.
Alisisitiza kuwa njia sahihi ni kuzungumza kutatua matatizo, akitolea mfano wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala kusikiliza maoni ya wananchi kila Alhamisi, akisema hapo ndipo mahali pa kupeleka kero.
Kwa sasa, taarifa za Wamachinga zinasema hali katika Soko la Kariakoo imerejea kuwa shwari tangu Novemba 3. Biashara zinaendelea kama kawaida katika soko hilo la kimataifa, ambalo katika siku za karibuni lilikuwa limeanzisha utoaji huduma wa saa 24.
Wamachinga wamewasihi wananchi na vijana kuendelea kuona athari za kuiga na kukurupuka.




