Breaking News

TANZANIA NA HUNGARY KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA ZA MAENDELEO

Dar es salaam - Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameishukuru Serikali ya Hungary kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mradi wa usambazaji maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria hadi Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.

Mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 55 (takribani shilingi bilioni 145) unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 200,000 wa Wilaya hiyo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2025, mara baada ya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó, Balozi Kombo alisema hatua hiyo ni mchango muhimu katika jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
“Tunaishukuru Serikali ya Hungary kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania. Kupitia ziara ya Mhe. Szijjártó, Hungary imetangaza kusaidia ujenzi wa mradi wa usambazaji maji Wilayani Biharamulo. Hungary ni miongoni mwa nchi zenye teknolojia ya kisasa ya uchujaji maji na usafirishaji wake kwa umbali mrefu,” alisema Kombo.

Ameongeza kuwa mradi huo unaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuboresha sekta ya maji nchini na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Waziri Kombo aliipongeza Serikali ya Hungary kwa kufungua ofisi za Ubalozi wake jijini Dar es Salaam, katika eneo la Masaki, akibainisha kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.

“Ufunguzi wa ofisi hizo ni heshima kwa Tanzania na ni alama ya kuimarika kwa ushirikiano wetu. Hatua hii itachochea biashara, uwekezaji, utalii, pamoja na huduma za kidiplomasia na kikonseli baina ya wananchi wa mataifa haya mawili,” alisema.