Breaking News

WATANZANIA WAASWA KUPIMA AFYA MARA KWA MARA KUKABILI MARADHI YA MOYO

Na Neema Mpaka - Jamii ya Watanzania imetakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kubaini mapema maradhi yasiyoambukiza, hususan ya moyo, kabla hayajasababisha madhara makubwa kwa miili na kuathiri uchumi wa familia.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Tulizo Shemu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Dar Group kwa kushirikiana na JKCI, ambapo wananchi walipatiwa huduma za kupima afya bure.

Dkt. Shemu amesema changamoto za moyo zimekuwa zikiongezeka na sasa siyo suala la watu wazima pekee, bali hata vijana na watoto wanaathirika. Amesema hapo awali maradhi hayo yalikuwa yakisumbua zaidi watu wenye miaka 70 na kuendelea, lakini kwa sasa hali imebadilika kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Kwa mujibu wa Dkt. Shemu, maradhi ya moyo yanaongoza kwa asilimia kati ya 60 hadi 70, na mara nyingi hutokana na lishe duni, kutofanya mazoezi na matumizi makubwa ya sukari. Ameongeza kuwa gharama za matibabu ya moyo ni kubwa, hivyo njia bora ya kujikinga ni kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na kupata ushauri wa kitaalamu.

Aidha, amebainisha kuwa JKCI imeimarisha huduma kwa kuongeza miundombinu, vifaa tiba na huduma za tiba utalii, huku kwa mwaka 2024/2025 taasisi hiyo ikiwafikia wananchi zaidi ya elfu 23 katika mikoa zaidi ya 20 na kuwapatia dawa na ushauri bure.
Kwa upande wake, Dkt. Eva Wakuganda, Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, amesema magonjwa ya moyo hayana rika, kwani watoto nao huzaliwa na matatizo hayo au kuyapata wakiwa wadogo. Ameeleza kuwa baadhi ya sababu za watoto kuzaliwa na matatizo ya moyo ni mama mjamzito kuwa na kisukari, uvutaji wa sigara, bangi na matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari.

Dkt. Wakuganda ametoa wito kwa wazazi jijini Dar es Salaam kuwapima watoto wao mara kwa mara kwani vipimo vya moyo kwa watoto huhitaji kufanyika mapema.

Ameonya pia kuwa shinikizo la damu ni miongoni mwa changamoto kubwa za moyo, na likiwa juu linaweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi. Dalili zake ni pamoja na miguu kuvimba, uchovu wa mara kwa mara na kupooza kwa viungo.