Breaking News

SERIKALI YA HUNGARY YAFUNGUA RASMI OFISI ZA UBALOZI NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Hungary kwa uamuzi wake wa kufungua Ofisi ya Dar es Salaam ya Ubalozi wa Hungary na kuitaja hatua hiyo kama alama ya kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Pongezi hizo zimetolewa na Mhe. Balozi Kombo kwenye Mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 29, 2025 na kumhusisha pia Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Amesema kuwa, ufunguzi wa Ofisi hizo ambazo zipo Masaki jijini Dar es Salaam ni heshima na upendeleo kwa Tanzania ambayo inadhihirisha namna ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ulivyoimarika na kwamba hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara, uwekezaji, utalii, mahusiano baina ya wananchi wa mataifa haya mawili na huduma nyingine za kidiplomasia na kikonseli zitakazotolewa na Ubalozi huo.

Kadhalika ameishukuru Serikali ya Hungary kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mradi wa usambazaji maji safi kutoka Ziwa Victoria katika Wilaya ya Biharamulo wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 55 utakaowafikia zaidi ya watu laki mbili Wilayani humo.
"Tunaishukuru Serikali ya Hungary kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania ambapo kupitia ziara ya Mhe. Szijjártó, Hungary imetangaza kusaidia ujenzi wa mradi wa usambazaji maji Wilayani Biharamulo. Hungary ni miongoni mwa nchi zenye teknolojia ya juu ya uchujaji maji na kuyapeleka kwenye masafa marefu kwa kutumia mitambo ya kisasa" alisema Mhe. Kombo.

Amesema mradi huu unaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya maji nchini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuondoakana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama.