Breaking News

WAZIRI KOMBO: MAJADILIANO YA SEKTA ZA UMMA NA BINAFSI NI NGUZO YA UKUAJI BIASHARA NA UWEKEZAJI

Dar es Salaam – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema majadiliano ya mara kwa mara kati ya sekta za umma na binafsi ni nguzo muhimu ya ukuaji wa biashara na uwekezaji, pamoja na kuwa msingi wa utawala bora na maendeleo endelevu.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao kati ya Watendaji Wakuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri Kombo amesema vikao hivyo ni fursa ya kupambanua changamoto zinazozikabili sekta binafsi na kuibua mikakati ya kuinua biashara, ushindani na kufungua fursa mpya kwa wafanyabiashara ndani ya Tanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Amezitaja sekta za kilimo, viwanda, uchukuzi na biashara za mipakani kuwa maeneo muhimu yanayohitaji mjadala wa kina kutokana na changamoto mbalimbali, huku akieleza kuwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) ndio waathirika wakuu wa vikwazo hivyo.
Aidha, Waziri Kombo amesema vikwazo visivyo vya kiforodha vimeendelea kurudisha nyuma juhudi za wanachama wa EAC katika kufanikisha malengo ya soko la pamoja, ambalo linapaswa kuruhusu biashara huru ya bidhaa, huduma na mtaji.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Kombo amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira thabiti ya kutekeleza sera zinazolenga kuboresha mazingira ya biashara, kukuza ushindani na kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi katika Jumuiya.