SWEDEN NA UNFPA WAWEZESHA VIJANA NA AKINA MAMA KITUO CHA YOMBO
Dar es Salaam - Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) wamezindua mpango wa uwezeshaji kwa vijana, hususan akina mama wa mara ya kwanza, wasichana balehe na vijana wenye ulemavu, kupitia Kituo cha Ufundi Stadi na Urekebishaji Yombo kilichopo Temeke.
Mpango huu, unaofadhiliwa kupitia msaada wa Mpango wa Nchi wa UNFPA wenye thamani ya Kronor milioni 30 za Kisweden (takribani dola milioni 2.8 za Marekani), unalenga kutoa mafunzo ya ufundi, pamoja na huduma za afya ya uzazi na haki za kijinsia (SRHR), sambamba na mkakati wa Serikali ya Tanzania wa kuwekeza katika rasilimali watu kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050.
“Kuwekeza kwa vijana, hasa akina mama wa mara ya kwanza, ni kuwekeza katika mustakabali wa Tanzania. Ushirikiano huu na Sweden unaleta fursa halisi za ujumuishi, uwezeshaji na heshima,” alisema Mark Bryan Schreiner, Mwakilishi wa UNFPA Tanzania.
Kupitia ufadhili huu, Kituo cha Yombo kimepatiwa vifaa muhimu vya mafunzo ikiwemo kompyuta, vifaa vya useremala, umeme, ususi, ufinyanzi, na utengenezaji viatu, pamoja na vifaa vya michezo na burudani. Vifaa hivyo vinawawezesha wanafunzi 260 waliowengi wakiwa wasichana kujipatia ujuzi wa kujitegemea kiuchumi na kijamii.
“Sweden inajivunia kushirikiana na Tanzania kuhakikisha vijana hasa wanawake na wale wenye ulemavu wanapata elimu na huduma za afya. Kuwapa vijana ujuzi na fursa ni kujenga jamii yenye usawa na nguvu zaidi,” alisema H.E. Charlotta Ozaki Macias, Balozi wa Sweden nchini Tanzania.
Mbali na mafunzo ya ufundi, zaidi ya akina mama wa mara ya kwanza 200 wakiwemo wenye ulemavu wananufaika kupitia mafunzo ya uongozi, ujasiriamali na huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana. Wengi wao wamejiunga na vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA) na mifumo ya kifedha midogo, wakibadilisha ujuzi waliopata kuwa kipato endelevu.
Mradi huo pia umeimarisha kituo cha afya cha Yombo, kinachohudumia zaidi ya watu 16,000 kutoka jamii jirani, kwa kukipatia vifaa tiba, kuboresha huduma za wagonjwa wa nje na kukarabati majengo.
Kwa Halima Suleman (17), mama kijana kutoka Temeke, mradi huu umeleta mabadiliko makubwa.
“Kabla ya kujiunga na Yombo, nilihisi maisha yangu hayana mwelekeo. Nilidorora shule, na kulea mtoto peke yangu kulikuwa kugumu. Sasa najifunza ushonaji na uongozi, na pia ninapata huduma za afya kwa ajili yangu na mwanangu. Sasa naamini naweza kujenga maisha bora kwetu,” alisema Halima.
Kisa cha Halima ni mfano wa matumaini kwa mamia ya akina mama vijana na vijana wengine wanaonufaika na mpango huu, wakibadilisha changamoto kuwa fursa.
Kwa kuchanganya elimu ya ufundi, stadi za maisha na huduma za afya, Kituo cha Yombo kimekuwa nguzo ya ujumuishi na maendeleo ya kijamii. Ushirikiano wa Sweden na UNFPA unathibitisha kwamba maendeleo jumuishi yanawezekana na kwa kuwekeza katika kila kijana, Tanzania inasonga mbele kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050 yenye usawa, ustahimilivu na ustawi kwa wote.






