MTIHANI WA TAIFA WA UPIMAJI DARASA LA NNE KUANZA KESHO
Dar es Salaam – Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kuwa jumla ya wanafunzi 1,582,140 wa Darasa la Nne kutoka shule 20,517 nchini wanatarakiwa kufanya Mtihani wa upimaji wa Taifa wa Darasa la Nne (SFNA) utakaofanyika tarehe 22 na 23 Oktoba, 2025.
Akizungumza mapema leo oktoba 21, 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Ally Mohamed, amesema kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 764,290 (asilimia 48.31) na wasichana ni 817,850 (asilimia 51.69).
Ameeleza kuwa asilimia 93.27 ya wanafunzi watafanya mtihani kwa Kiswahili, huku asilimia 6.73 wakitumia Kiingereza, kutegemeana na lugha ya kufundishia inayotumika katika shule zao.
Aidha, jumla ya wanafunzi 5,750 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa, wakiwemo wenye uoni hafifu, wasioona, wenye ulemavu wa kusikia, ulemavu wa akili, na ulemavu wa viungo.
Prof. Mohamed amebainisha kuwa mwaka huu, mtihani utafanyika kwa mara ya kwanza chini ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) pamoja na mitaala iliyoboreshwa.
Wanafunzi watapimwa katika masomo sita ya Sayansi, Hisabati, Jiografia na Mazingira, Sanaa na Michezo, Kiswahili, Lugha ya Kiingereza na Historia na Maadili ya Tanzania.
Alisema pia Kutakuwa na masomo matatu ya hiari Kifaransa, Kiarabu, na Kichina ambapo kila mwanafunzi atachagua somo moja tu.
Akifafanua lengo la mtihani huo, Prof. Mohamed amesema unalenga kupima uwezo wa wanafunzi katika Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (3Rs) pamoja na uelewa wao katika masomo wanayosoma. Matokeo yake yatasaidia walimu na wakuu wa shule kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Ameongeza kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika, ikiwemo usambazaji wa karatasi za mitihani na vifaa husika katika halmashauri zote nchini, pamoja na maandalizi maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa mujibu wa Prof. Mohamed, Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zimeelekezwa kuhakikisha vituo vyote vya mitihani vinakuwa salama na vinafuata taratibu za NECTA.
NECTA pia imewahimiza wasimamizi wa mitihani kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu, umakini na weledi, na kuhakikisha wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum wanapata fursa sawa. Wanafunzi wasioona watapatiwa karatasi za maandishi ya nukta nundu (Braille), wenye uoni hafifu watapewa nakala zenye maandishi makubwa, na wote wenye mahitaji maalum watapewa muda wa ziada dakika 20 kwa kila saa ya somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa ya masomo mengine.
Baraza limewakumbusha wanafunzi kuzingatia kanuni za mitihani na kuepuka udanganyifu wa aina yoyote, likisisitiza kuwa mwanafunzi atakayebainika kudanganya matokeo yake yatafutwa kulingana na kanuni za mitihani.
Aidha, wamiliki na wakuu wa shule wamekatazwa kusimamia mitihani ndani ya vyumba vya mitihani, na NECTA imeonya kuwa kituo chochote kitakachokiuka usalama wa mitihani kitapokonywa usajili wake.
NECTA imewaomba wananchi wote kushirikiana katika kudumisha amani na usalama wakati wa kipindi cha mitihani, na kuzuia watu wasiohusika kuingia kwenye maeneo ya shule wakati wa mtihani.
Kwa kumalizia, Prof. Mohamed amewataka wadau wa elimu na wananchi kwa ujumla kusaidia kufanikisha uendeshaji mzuri wa mtihani huo, na kuripoti udanganyifu wowote kupitia namba ya simu 0759 360 000 au barua pepe esnecta@necta.go.tz.
Baraza la Mitihani la Taifa linawatakia wanafunzi wote mafanikio mema katika Mtihani wa huo wa upimaji wa Taifa wa Darasa la Nne utakaofanyika tarehe 22 na 23 Oktoba, 2025.



