Breaking News

NEEC YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UWEZESHAJI WA KIUCHUMI

Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Neema Mwakatobe akizungumza katika ufunguzi wa warsha kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu majukumu yake na namna linavyotekeleza shughuli za uwezeshaji nchini mapema leo oktoba 10, 2025 jijini dar es salaam.
Mkurugenzi wa huduma za taasisi kutoka Baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC), Bwana Gwakisa Bapala akiwasilisha mada katika warsha kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi kiuchumi mapema leo oktoba 10, 2025 jijini dar es salaam.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), Bw. Selemani Msuya akifafanua jambo Wakati akiongea katika ufunguzi wa warsha hiyo kuhusu umuhimu wake kwa waandishi wa habari mapema leo oktoba 10, 2025 jijini dar es salaam.
Washiriki wa warsha hiyo waandishi kutoka vyombo vya habari mbalimbali vya habari.


Dar es salaam - Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeanza kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari nchini ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya uwezeshaji na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kupitia Baraza hilo.

Kupitia warsha maalum iliyowakutanisha waandishi wa habari, NEEC imeeleza dhamira yake ya kutumia nguvu ya vyombo vya habari katika kufikisha elimu ya uwezeshaji kwa Watanzania wengi zaidi.

Akizungumza katika warsha hiyo, Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Neema Mwakatobe, alisema ushirikiano huo utasaidia jamii kupata taarifa sahihi kuhusu kazi na majukumu ya Baraza hilo, pamoja na kuelewa fursa zilizopo za kiuchumi nchini.

“Tunatambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kuelimisha jamii. Kupitia ninyi, wananchi wataweza kujua wapi pa kupata msaada wanapokutana na changamoto za kiuchumi, na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” alisema Bi. Mwakatobe.

Alibainisha kuwa NEEC ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, na jukumu lake kuu ni kufuatilia na kutathmini shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinazotekelezwa na taasisi mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Bi. Mwakatobe, Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilianzishwa mwaka 2004, ikifuatiwa na Sheria ya mwaka 2005 iliyoanzisha rasmi Baraza hilo kwa lengo la kuratibu na kuhakikisha Watanzania wanashiriki ipasavyo katika uchumi wa nchi.
Ameongeza kuwa NEEC hufanya kazi kwa karibu na wizara, taasisi na wadau wa maendeleo wanaotekeleza programu za kuwawezesha wananchi, huku ikihakikisha utekelezaji wa mipango hiyo unawafikia walengwa.

“Ni jukumu letu kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo za uwezeshaji. Tunafuatilia wadau wote wanaotekeleza shughuli hizi na kutoa taarifa kwa umma ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), Bw. Selemani Msuya, aliishukuru NEEC kwa kutoa elimu hiyo muhimu kwa wanachama wa chama hicho.

Tunaishukuru NEEC kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari. Kupitia semina hii, wanachama wetu watakuwa mabalozi wazuri wa kufikisha taarifa za uwezeshaji kwa wananchi,” alisema Bw. Msuya.

Aliongeza kuwa JOWUTA ina wanachama zaidi ya 300 nchini, wakiwemo zaidi ya 150 kutoka mkoa wa Dar es Salaam, na akaomba NEEC kuendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa waandishi wa habari wa mikoa mingine ili kuongeza uelewa wa umma.

Warsha hiyo ilihusisha mada mbalimbali zikiwemo Mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, Ushiriki wa Watanzania katika uchumi, Utoaji wa huduma za biashara, na Muongozo wa watoa huduma za biashara.

Kwa ushirikiano huu mpya kati ya NEEC na vyombo vya habari, inatarajiwa kuwa wananchi wengi zaidi watapata maarifa sahihi kuhusu fursa za kiuchumi, jambo litakalosaidia kukuza ushiriki wao katika kujenga uchumi wa Taifa.