EWURA YATANGAZA BEI MPYA ZA MAFUTA, PETROL BEI JUU, MZOZO WA KIVITA KATI YA MAREKANI, ISRAEL NA IRAN CHANZO
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazoanza kutumika kuanzia leo Jumatano, Aprili 1, 2026 ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la bei ikibainishwa kuwa ni kutokana na athari za mzozo wa kivita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran ulioibuka Februari 28, 2026.
Katika taarifa yake, EWURA imeeleza kuwa mashambulizi katika visima vya mafuta, maghala na viwanda vya kusafisha mafuta Mashariki ya Kati pamoja na kufungwa kwa Lango la Hormuz—linalopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta duniani, vimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kuathiri pia gharama za uagizaji nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa bei mpya:
Dar es Salaam: Petroli Sh 3,820, Dizeli Sh 3,806, Mafuta ya Taa Sh 3,684
Tanga: Petroli Sh 3,881, Dizeli Sh 3,867, Mafuta ya Taa Sh 3,745
Mtwara: Petroli Sh 3,912, Dizeli Sh 3,898, Mafuta ya Taa Sh 3,777 huku maeneo mengine Petroli ikiwa ni zaidi ya Sh. 4000
EWURA imesisitiza kuwa wafanyabiashara wote wa mafuta nchini wanapaswa kuuza kwa bei zinazoonyeshwa kwenye mabango ya vituo vya mafuta, na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka.
Aidha, mamlaka hiyo imewataka wananchi kutumia mafuta kwa uangalifu na ufanisi kutokana na athari za kimataifa zinazoendelea, huku ikiendelea kuchukua hatua za kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini hauathiriki.
Bei hizo zimepanda ikiwa ni tofauti na Bei zilizotangazwa tarehe 4 Machi 2026 ambayo maeneo mengi ilikuwa ni Sh 2864 hadi 2959.










